Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Elimu ni nyenzo muhimu katika kumsaidia mwanadamu kumudu na kutawala mazingira yake na hivo kuboresha maisha yake. Mtu anapopata maarifa, stadi na ujuzi katika maisha yake, inakuwa ni msaada mkubwa katika kuendesha maisha kwa kuwa yale aliyojifunza anayatumia katika kukabiliana na maisha. Kutokana na umuhimu wa elimu, haki ya kupata elimu ni miongoni mwa haki za binadamu ambazo kimsingi kila mwanadamu anayo haki ya kupata elimu na yeyote anayehusika kukwamisha anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kimsingi, elimu ni ghali, ni gharama, ndiyo maana wahenga walisema “Ikiwa unaona elimu ni ghali basi jaribu ujinga ambao hauna gharama kabisa.”
Kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na utoaji wa elimu, serikali, asasi zisizo za kiserikali, mashirika na wananchi wamekuwa wakisaidia kuchangia maendeleo ya elimu kwa kutoa fedha, sare za wanafunzi, kalamu, madaftari, kompyuta, madawati, meza, viti au vifaa vya ujenzi na michezo ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na wanafunzi wanajifunza katika mazingira mazuri yanayochochea uelewa.
Serikali kama mdau namba moja katika maendeleo, imewajibika ipasavyo kutekeleza sera ya elimumsingi bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita ili wanafunzi waweze kusoma bila kikwazo chochote.
Pia, serikali imefanya kazi kubwa kuboresha miundombinu ya shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kwa kujenga madarasa, ofisi za walimu, vyoo, maabara, mabweni, mabwalo na nyumba za walimu. Vilevile, kuajiri walimu, wakufunzi na wahadhiri ili kuweza kuwafundisha wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu.
Aidha, serikali pia inatoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu ili kuweza kumudu gharama kubwa za elimu ya juu kama vile ada, chakula, malazi, vitabu, nauli, mafunzo kwa vitendo na fedha za kujikimu. Hapa kwenye gharama za kugharimia elimu ya juu ndipo ulipo msingi wa mjadala wangu kwa leo.
Ili kuratibu vyema zoezi la utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo, serikali ilianzisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) mwaka 2004. Bodi hii inawajibika katika kupokea maombi, kuyachakata, na mwisho kutoa majina ya waombaji waliokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo. Kwa wale waliokidhi kupata mikopo, hupata taarifa juu ya asilimia za mikopo walizopata ili kujua gharama nyingine wanazopaswa kuchangia ili kuongezea na hatimaye kulipa gharama zote wanazopaswa kulipa vyuoni.
Mathalani, mwanafunzi aliyepata mkopo wa asilimia 80, na ada ya kozi yake ya chuo ni shilingi milioni moja kwa mwaka, basi bodi ya mikopo itamlipia mnufaika huyo shilingi laki nane na yeye mnufaika wa mkopo atapaswa kuongezea shilingi laki mbili ili kukamilisha milioni moja ya ada inayotakiwa kulipwa kwa mwaka.
Ikumbukwe kuwa Bodi ya Mikopo haitoi msaada wa fedha bali inakopesha wanafunzi kwa mkataba kuwa mnufaika wa mkopo atakapohitimu masomo yake, basi aanze kurejesha mkopo uliotumika kumsomesha ili fedha hizo zitumike kusomesha wengine wenye uhitaji wa mkopo kama ambavyo mnufaika huyo alisomeshwa kwa fedha walizorejesha wenzie waliomtangulia kusoma.
Kwa hiyo, kila mnufaika wa mkopo, anapaswa kuzingatia kuwa anawajibika kurejesha mkopo huo anapohitimu masomo yake hasa baada ya kujiajiri au kuajiriwa. Kwa walioajiriwa katika sekta binafsi au umma wanapaswa kurejesha asilimia 15 ya mshahara wao wa kila mwezi na kwa wale waliojiajiri wanayo fursa ya kuwasiliana na Bodi ya Mikopo na kuweka utaratibu wa kiwango cha fedha wanachoweza kurejesha kila mwezi kutokana na vipato vyao vya kujiajiri.
Ili kuongeza wigo wa marejesho ya fedha kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, HESLB imekuja na kampeni iitwayo “Fichua – Kuwa Hero wa Madogo” ili kuwamulika na kuwafichua wanufaika wa mikopo ambao tayari wameshapata ajira lakini hawajaanza kurejesha fedha zilizowasomesha katika taasisi mbalimbali za elimu. Kampeni hii ni maalumu ya kuwasaka wadaiwa sugu 50,000 ambao ni wanufaika wa mikopo ili kukusanya shilingi bilioni 200.
Kampeni hii ya Fichua imezinduliwa rasmi Juni 28, 2024 na itaendeshwa kwa kipindi cha miezi miwili ikiwa na nia njema kabisa ya kuongeza wigo wa makusanyo ya fedha kwa kuwafichua wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao tayari wameshapata kazi lakini bado hawajaanza kurejesha mikopo ya elimu ya juu. Katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa HESLB, Dk. Bill Kiwia amesema: “Kampeni hii inalenga kuwashirikisha wananchi kutimiza jukumu la kizalendo la kuwafichua wadaiwa wa HESLB wenye kipato lakini hawajitokezi na kuanza kurejesha.”
Kimsingi, upo umuhimu wa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kuwa wazalendo kwa kutambua kuwa fedha zilizotumika kuwasomesha ni zao la wanufaika wenzao ambao kwa moyo wa upendo kabisa waliamua kurejesha mikopo hiyo na ndipo zikapatikana fedha za kuwasomesha wao. Hivyo basi, hata wao wanalo jukumu la kurejesha fedha hizo hata kama bado hawajaanza kukatwa moja kwa moja kupitia mishahara yao au kupitia ajira binafsi walizonazo.
Dk. Kiwia amewasihi wananchi kuwafichua wadaiwa sugu wa mikopo ili kuwezesha wanufaika wengi zaidi kunufaika na mikopo ya elimu ya juu. “Ili kutoa taarifa za wadaiwa, mwananchi anapaswa kutuma jina la mnufaika, chuo alichosoma, eneo analofanyia kazi, jina la kampuni anayofanyia kazi au anayomiliki na eneo ilipo kampuni hiyo,” amesisitiza Dk. Kiwia. Hivyo, wananchi tuiunge mkono HESLB kwa kuwafichua wadaiwa sugu ili kuongeza makusanyo ya bodi na hatimaye vijana wengi zaidi waweze kupata fursa ya kusoma elimu ya juu.
Ndugu msomaji wangu, kwa leo niishie hapa.
Itaendelea.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462