Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amezindua rasmi akademia ya michezo inayoitwa “one Tanzanite Football Academy” itakayotoa mafunzo na uendelezaji wa vipaji mbalimbali vya michezo.
Akizindua akademia hiyo leo Julai 13, 2024 katika viwanja vya Gymkana-Posta, Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Msigwa ameipongeza One Tanzanite Football kwa kufanya uwekezaji katika sekta ya michezo akieleza kuwa uwekezaji huo unaunga mkono ndoto na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza michezo nchini.
Amesema Serikali inaunga mkono juhudi hizo za wadau wa Sekta binafsi wanaojitokeza kuwekeza kwenye Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo akibainisha kuwa One Tanzanite Football Academy itahusika na Vijana wenye umri wa miaka 6 hadi 16 kwa ajili ya maandalizi ya ACON 2027
Katika hatua nyingine ameliagiza Baraza la Michezo Tanzania (BMT lifanyie kazi suala la miundombinu na mikakati ya kupata maeneo kwa ajili ya akademia zinazoanzishwa na sehemu za kufanyia mazoezi.