MKURUGENZI wa Manispaaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,amesema kuwa wameokoa sh.milioni 26 kati ya bilioni 1.4 zilizopangwa kutekeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa 44 ya shule za sekondari,matundu 72 ya vyoo,ukamilishaji wa maboma 15, ununuzi viti na meza 2,750.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya elimu wilayani humo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,leo amesema mwaka wa fedha 2023/24 waliidhinishiwa sh. bilioni 2.4 za kujenga madarasa 80 kati ya hizo ilipokea sh. bilioni 1.4 za madarasa 44,matundu 72 ya vyoo,kununua seti ya viti meza 2,750 za wanafunzi na kukamilisha maboma 15 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.
“Miradi hiyo imekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya sh.bilioni 1.394 kati ya bilioni 1.4 na hivyo tumeokoa sh. milioni 26 ambazo zimetumika kutengeneza viti 23 vya walimu,kukamilisha madarasa 4,ukarabati wa matundu 6 ya vyoo na ofisi mbili,ujenzi wa matundu mawili ya vyoo vya walimu na ujenzi wa ofisi ya walimu,”alisema Wayayu.
Mkurugenzi huyo Ilemela ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo,kuendelea kutoa fedha pia wananchi wa Wilaya ya Ilemela kwa kushirikiana na serikali kuleta maendeleo.
“Mkurugenzi niwapongeze kwa usimamizi wa bilioni 1.4 mkaokoa milioni 26, kwa mjini ni nadra kufanya kazi chenchi ikabaki,miradi haiishi fedha zinaliwa halafu itakamilishwa kwa mapato ya ndani,kwa kitendo hiki Ilemela mmenifurahisha sana, msimamo wa serikali si lazima fedha zilizotengwa zitumike zote,tunaweza kuokoa zikafanya kazi nyingine,”amesema.
Mtanda amesema maeneo mengine fedha hizo zingeliwa ikabaki kazi ya kufikishana na TAKUKURU,hivyo serikali imedhamiria kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu pia kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo kulipa madai ya malimbikizo yao.
“Walimu endeleeni kushirikiana na serikali na muwe wavumilivu mfanye kazi bila manung’uniko kwa sababu maendeleo yanapozidi changamoto zingine zinaibuka.Pia bilioni 5.4 za maendeleo angalieni majengo yaliyojengwa na wananchi katika shule hii (Lumala) yakamilishwe kwa mapato ya ndani yafanane na mapya,”ameagiza mkuu huyo wa mkoa.
Aidha Mtanda amesema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na miradi ya maendeleo iliyofanywa na Rais Dk.Samia,salamu za wananchi wa Ilemela amezipokea na kuahidi kumfikia Rais ili kumtia moyo aendelee kuleta fedha za maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Ilemela,Dkt,Angeline Mabula amemshukuru na kumwombea maisha marefu Rais Samia kwa kumwaga fedha nyingi za maendeleo jimboni humo, changamoto ni mifumo kuchelewesha fedha kutolewa.
“Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi,fedha zinamiminika hata la kusema sina, Ilemela ya miaka 10 iliyopita haifanani na ya leo.Bilioni 4.61 isingekuwa mdudu mfumo kazi ingeshafanyika pia bilioni 1.94 zimechelewa kutoka sababu ya mfumo, unachelewesha maendeleo,”amesema.
Dkt.Mabula ameomba serikali kuboresha mifumo kazi ifanyike haraka sababu mifumo ni kikwazo,fedha zinazoidhinishwa hazitoki na hivyo kuchelewesha maendeleo.