Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ametoa saa 48 kuondoka katika wilaya yake kwa kampuni inayofanyashughuli zake kwa njia ya mtandao ya Alliance in Motion Global kwa kukusanya vijana 80 bila kuwa na vibali vya kisheria.
Kampuni hiyo ambayo imekosa uhalali wa kufanya kazi wilayani Njombe imekuwa ikikusanya vijana toka mikoa mbalimbali na kuwatoza fedha kiasi cha shilingi laki sita ili kujiunga na kisha kufundishwa masuala ya afya na virutubisho lishe pamoja na fursa za kibiashara pasina kuwa na usajiri wa kisheria.
Kutokana na hali hiyo mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amechukua hatua ya kuwafurusha katika wilaya yake kwa kuwapa saa 48 na kuwataka kufuata taratibu za kisheria kuendesha mambo yao.
Awali mamlaka za serikali kupitia Ofisa Afya wa Halmashauri ya mji wa Njombe Inosensia Mtega anasema shughuli wanazofanya vijana hao hazijazingatia maelekezo ya wataalamu wa Afya na hawajatoa kibali chochote.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Njombe Isack Mapunda anakiri kuwapo kwa ujanja ujanja wa kupata baadhi ya nyaraka ambazo hakuna mamlaka ya serikali iliyozitambua huku Ofisa kodi wa TRA Mkoa wa Njombe Pyson Mwansasu akisema leseni waliyoanza kufuatilia vijana hao haikukamilishwa taratibu zote.
Kituo hiki kimezungumza na baadhi ya vijana hao akiwemo kiongozi wao Bahati Ndundo wanakiri kunufaika na mfumo huo wanaouendesha huku wakiahidi kwenda kufuata taratibu zote za kisheria za kusajili kampuni.