Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini Bi. Samia Chande (wa kwanza kushoto), Afisa Mkaguzi TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Bw. Enock Emmanuel (wa kwanza kulia) wakitoa elimu ya maboresho ya mfumo wa mita za Luku Mfanyabiashara wa kukoboa nafaka katika zoezi la kuelimisha wateja lililofanyika leo Julai 12, 2024 katika Soko la Tandale na Mazense, Dar es Salaam.
Maafisa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini wakitoa elimu ya maboresho ya mfumo wa mita za Luku kwa wateja wake wakiwemo wananchi na wafanyabiashara wanaokoboa nafaka mbalimbali ikiwemo Mahindi na Mpunga katika zoezi la kuelimisha wateja lililofanyika leo Julai 12, 2024 katika Soko la Tandale na Mazense, Dar es Salaam.
……………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini limetoa elimu ya maboresho ya mfumo wa mita za Luku kwa wateja wake wakiwemo wananchi na wafanyabiashara wanaokoboa nafaka mbalimbali ikiwemo Mahindi na Mpunga katika Soko la Tandale na Mazense.
Akizungumza leo Julai 12, 2024 wakati akitoa elimu ya maboresho ya mfumo wa Luku kwa wateja katika Kata ya Tandale na Mazense, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Bi. Samia Chande, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wateja wanakuwa na uelewa mkubwa wa maboresho mfumo wa mita za luku unaotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 22, 2024.
Bi. Chande amesema kuwa kutokana na umuhimu wa maboresho ya mfumo wa luku wameona ni vizuri kutoka Ofisini na kuwatembelea wateja wao ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.
“Tumewaelimisha taratibu za kufata ili waweze kufanya maboresho ya mfumo wa luku pamoja na kuwapatia mawasiliano yetu : namba ya simu ya mkoani 0756 251 753 ili watakapopata changamoto tuweze kuwafikia kwa haraka” amesema Bi. Chande.
Amesema kuwa utaratibu wa kutoa elimu kwa kuwafikia wateja maeneo yao ni sehemu ya utaratibu wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Bi. Chande amesema kuwa lengo la maboresho ni kuzijengea uwezo mita za luku ziweze kuwa na ufanisi ambapo mteja atapewa tarakimu zenye makundi matatu na kuingiza katika luku yake kwa ajili ya maboresho.
Afisa Mkaguzi TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Bw. Enock Emmanuel pamoja Afisa Huduma kwa Wateja katoka Mkoa huo Bw. Jimmy Luberty wamesisitiza umuhimu wa wateja kufanya maboresho ya mita za luku ili kuleta tija katika upatikanaji wa huduma ya umeme.
Nao wateja wakiwemo Bw. Abdallah Kombo pamoja na Bi Neema Moshi wamepongeza huduma bora inayotolewa na TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kuwatembelea kwa ajili ya kutoa elimu, kusikiliza changamoto zao, huku wakitoa wito utaratibu huo uwe endelevu.