Bohari ya Dawa MSD imeendelea kuhakikisha mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za
afya yanatimizwa kwa mujibu wa maombi yao kutokana na kuimarika kwa utendaji.
Hayo yanaelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa Bw. Tukai Mavere wakati alipokutana na wahariri wa habari hivi karibuni jijini Dodoma ambao walikuwa katika ziara ya taasisi hiyo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayofanywa na MSD.
Hadi kufikia Juni 2024, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika
kutekeleza majukumu yake ambapo mafanikio hayo yamepatikana katika maeneo mbalimbali
Amesema kuwa kuongezeka kwa utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za
afya (Dawa,Vifaa,Vifaa Tiba na Vitendanishi) kumefanya kazi ya kusambaza bidhaa hizo za afya kuwa nyepesi kufanya malengo ya kuhudumia wadau wao kwenda vizuri.
Anasema Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za
afya yanatimizwa kwa mujibu wa maombi yao. Kutokana na kuimarika kwa utendaji.
“Utimizaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma za afya
umeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2022/23 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2023/24 na hivyo bidhaa nyingi kuweza kupatikana kupitia MSD, ” Anasema Tukai Mavere
Ameongeza kuwa sambamba na hilo, MSD imeendelea kufanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba
vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi nchini kama mashine za kusafisha damu (Dialysis Machine), MRI, CT- Scan, Ultrasound, Digital X-Ray pamoja na vitendanishi vyake.
Ametanabaisha kuwa uwepo wa vifaa hivi unawezesha utambuzi
wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi.
Mizunguko ya Usambazaji wa Bidhaa za Afya pia imeongezeka katika kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kufanikisha
usambazaji wa bidhaa za afya nchi nzima kwa mizunguko sita (vituo kupelekewa bidhaa kila baada ya miezi miwili) kutoka mizunguko minne (vituo kupelekewa bidhaa kila baada ya miezi mitatu) na hivyo kupelekea vituo kuwa na dawa toshelevu muda mwingi.