……..
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MRADI wa maji wa Mogitu Gehandu wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, utawanufaisha wakazi wa kata mbili za Mogitu na Gehandu wilayani Hanang’ mkoani Manyara na baadhi ya vijiji vya mkoa wa Singida.
Pindi mradi huo wa maji wa Mogitu Gehandu wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wenye thamani ya Sh8 bilioni ukikamilika unatarajia kunufaisha watu 25,217.
Akisoma taarifa ya mradi huo wakati mwenge wa uhuru ukiweka jiwe la msingi Julai 12, meneja wa RUWASA wilaya ya Hanang’ mhandisi Hurbert Kijazi amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili.
“Awamu ya kwanza imeshakamilika na watu zaidi ya 16,000 wananufaika hivi sasa ila ukikamilika watu 25,217 wanatarajia kunufaika,” amesema mhandisi Kijazi.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2024, Geofrey Mnzava amesema mradi huo ukikamilika unapaswa kutunza ili unufaishe kizazi cha sasa na kijacho.
“Kina mmoja anapaswa kutunza vyanzo vya maji visiharibiwe ili kuondoa kero ya upatikanaji wa maji, nawapongeza RUWASA kwa namna mnavyotekeleza miradi yenu,” amesema Mnzava.
Mkazi wa kijiji cha Mwahu kata ya Gehandu, Daniel Bahari akizungumza baada ya mwenge wa uhuru kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo amesema hivi sasa wanafuata mbali huduma ya maji kwenye mkoa jirani wa Singida.
“Nawapongeza Ruwasa kwa hatua hii kwani ukikamilika kwake utaondoa kero ya maji kwa wananchi wa maeneo haya ambao baadhi wanatumia mikokoteni kwenda mbali kufuata maji mkoa wa Singida,” amesema.
Amesema wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa wa ukosefu wa maji eneo hilo hivyo mradi ukikamilika utakuwa nafuu kwao.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Christina Timotheo amesema ni muda mrefu eneo hilo halijapata huduma ya maji ila kupitia Ruwasa watanufaika na huduma hiyo.
“Tunatumia muda mrefu kufuata maji Singida ila mradi huu ukikamilika utawasaidia wananchi wengi na dhana ya serikali kumtua ndoo mama kichwani itaonekana,” amesema.
Amesema wananchi wa eneo hilo wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa mradi huo kwani watafanya shughuli za kiuchumi kuliko kutumia muda mrefu kufuata huduma ya maji mbali.