NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imesema ipo katika mpango wa kuingia makubaliano na nchi ya India katika sekta ya kilimo na mafuta ya kula ya Alizeti kwani wamekuwa wakifanya vizuri katika masoko mbalimbali duniani.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa siku maalum ya India (India day) iliyofanyika katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere,
Mkurugenzi wa TanTrade, Bi. Latifa Khamis, amesema kuwa India ni wakulima wazuri wa mazao mbalimbali ikiwemo mchele.
Amesema kuwa katika maonesho ya sabasaba ya mwaka huu wafanyabiashara 40 kutoka nchini India wamekuja nchini ambapo wametembelea viwanda mbalimbali nchini na kushirikia katika mkutano wa wafanyabiashara kati ya India na Tanzania.
“Wafanyabiashara hao wanania ya kuwekeza nchini na TanTrade itahakikisha inawaunganisha na watu wengine ili waweze kufikia lengo la kufanya uwekezaji” amesema Bi. Khamis.
Amesema kuwa Tanzania wanaangalia jinsi gani wanaweza kuongeza thamani mafuta ya kula haşa ya alzeti, kwani India wapo tayari kuwekeza na kufanya uchakataji.
“TanTrade jukumu letu ni kuhakikisha fursa hizo zinakuja na kupitia programu tunazofanya katika maonesho tunahakikisha fursa walizokuja nazo wafanyabiashara kutoka nje zinabaki hapa nchini,” amesema
Mwenyekiti wa Bodi
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Binlith Mahenge, amesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kusajili miradi 730 kutoka nchini India ambayo inathamani ya dola za marekani zaidì ya Milioni 4000.
“Nchi ya India kuna wawekezaji wakubwa wanataka kufanya uwekezaji hapa nchini” amesema.
Kamishna wa Bima Bahayo Sakware amesema kuwa kupitia maonesho ya mwaka huu wanaendelea kutoa wito kwa wawekezaji kufanya uwekezaji kwenye maeneo ya bima za kilimo, afya kwa sababu serikali kupitia uongoziwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unatarajia kuona watanzania wakiwa na afya njema na uchumi imara.
“Tunahitaji makampuni mengi yenye uzoefu tofauti tofauti kuja kufanya biashara nchini na tunawakaribisha wote kwenye maonesho haya,tumetoa mada kuhusu fursa zilizopo kwenye kwenye sekta ya bima” amesema.