Mbunge wa Viti Maalum, Suma Fyandomo(kushoto) akikabidhi kadi za Bima ya Afya kwa Mwenyekiti wa Balaza la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake(UWT) Mbeya mjini, Suma Mwaikambo kwenye kikao cha Balaza la kawaida kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini humo.(Picha na Joachim Nyambo).
Mbunge wa Viti Maalum, Suma Fyandomo(katikati) akiwa na Wajumbe wa Balaza la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Mbeya mjini (UWT) baada ya kikao cha Balaza la kawaida kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini humo.(Picha na Joachim Nyambo).
………………
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
BIMA za Afya zenye thamani ya Shilingi milioni 15 zimetolewa na mbunge wa vitu maalumu, Suma Fyandomo kwa kaya 500 za wenye uhitaji mkoani Mbeya lengo likiwa ni kuziwezesha kuwa na uhakika wa matibabu.
Miongoni mwa kaya zitakazonufaika na msaada huo ni pamoja na za wajumbe wote wa Baraza la Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT) mkoani Mbeya.
Fyandomo amekabidhi kadi hizo kwenye Kikao cha Baraza la kawaida la UWT kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini humo.
Akikabidhi msaada huo mbunge huyo amesema jumla ya wananchi 3,000 watanufaika na bima hizo kutoka kaya 500 kwa maana ya kila kaya moja kuwa na jumla ya wanufaika sita.
Amesema ameupa kipaumbele msaada wa bima ya afya kutokana na familia nyingi kukabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa kupata matibabu kwa wakati pale inapotokewa kupatwa na mgonjwa.
Amesema kutokana na hali duni za kimaisha zipo kaya ambazo hujikuta zinapoteza wapendwa wao kutokana na vifo vinavyotokana na kuchelewa kupata matibabu au kuyakosa kabisa kwakuwa hazikuweza kumudu gharama zilizohitajika.
Pia alisema zipo kaya zilizojikuta zinaingiwa na umasikini baada ya kulazimika kuuza rasilimali muhimu ikiwemo mashamba, mifugo au nyumba ili kugharamia matibabu ya wagonjwa wao.
Aliongeza kuwa kwa kuwa na kadi za bima ya afya ni wazi kuwa familia zitaweza pia kuwa na nafasi kubwa ya uzalishaji kiuchumi kwakuwa hazitokuwa na afya ya kusuasua kwani watu wake watatibiwa mara moja na kurejea kwenye majukumu yao ya kawaida.
Akipokea kadi hizo, Mwenyekiti wa UWT Mbeya mjini, Suma Mwaikambo alimpongeza mbunge huyo kwa kuwa na moyo wenye kuwajali wanawake walio wajumbe wa jumuiya hiyo akisema kwa msaada huo ana imani familia zao zitakuwa salama kwenye upande wa afya kwakuwa wao ndiyo wasimamizi wa karibu kwenye jamii wanazotoka.