Singida
Naibu Waziri wa Madini,Dkt. Steven Kiruswa ameupongeza mkoa wa Singida kwa kuvuka lengo walilopangiwa kukusanya kwa asilimia 145.
Dkt.Kiruswa alibainisha hayo Julai 10, 2024 katika ziara yake ya kikazi kwa wachimbaji wadogo wa madini inayoambatana na ukaguzi wa miradi ya kimkakati inayosimamiwa na mgodi wa kati wa uchimbaji dhahabu wa Singida Gold Mine pamoja na kupokea taarifa juu ya uwajibikaji wa mgodi kwa Jamii inayozunguka mgodi huo (CSR).
Akizungumza baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Afisa Madini Mkazi mkoa wa Singida Mha. Sabai Nyansiri , Dkt. Kiruswa alisema kuwa awali mkoa wa Singida ulipewa lengo la makusanyo TZS 12bilioni lakini hadi kufunga mwaka wa fedha 2023/24 Ofisi hiyo ilikuwa imekusanya 18bilioni. Hii ni kutokana na juhudi zilizowekwa na huu ni mfano wa kuigwa.
Pia , Dkt.Kiruswa aliupongeza Mgodi huo kwa utekelezaji wa Mpango wa Wajibu wa Mgodi kwa Jamii inayozunguka mgodi kwa kufanikisha mradi wa ujenzi wa nyumba za jamii , madarasa ya shule na kuweka mifumo mizuri ya utunzaji mazingira katika eneo la mgodi.
Kwa upande wake , Mkuu wa wilaya ya Ikungi Thomas Apson aliishukuru wizara ya madini kupitia miradi ya kimkakati katika wilaya ya Ikungi na aliomba wizara kuendelea na utafiti wa madini ili kugundua maeneo mapya ya madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa uhakika bila kuleta migogoro .
Katika ziara hiyo Dkt.Kiruswa aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Madini , Tume ya Madini , viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa.