Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho Dk. Omar Dadi Shajak, amesema jukumu la msingi kwa vyuo vinavyosomesha madaktari na wauguzi, ni kuwaandaa wanafunzi kuwa wabobezi wa kweli, kwani kazi yao inahusika moja kwa moja na uhai wa wanadamu, ambao haupaswi kuchezewa.
Akizungumza na gazeti hili chuoni hapo, Mwenyekiti huyo alisema miongoni mwa malengo ya kuanzisha chuo hicho, ni kuisaidia serikali kuwa na vituo vya afya na hospitali vinavyotoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema dhamira hiyo inaakisi juhudi za serikali kuandaa kizazi kilicho imara kiafya kitakachomudu kufanya kazi ili kuinua uchumi na ustawi wa nchi na wananchi wake.
Dk. Shajak alifahamisha kuwa, chuo hicho kilichopata usajili wa NACTVET Agosti 10, 2022, kinafundisha fani mbili, ufamasia na uuguzi/ ukunga ngazi ya Stashahada.
Alisema, kikiwa katika mwaka wa pili sasa, chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 506 wanawake na wanaume, ufamasia 442 na uuguzi/ukunga 64.
“Lengo letu kuu ni kutoa elimu bora itakayowajenga wanafunzi wetu vizuri ili wakitoka hapa wakubalike katika soko la ajira au kujiajiri wenyewe. Na katika hili tuko makini kuepusha udanganyifu wakati wa mitihani ili wasiende kucheza na uhai wa watu,” alifafanua.
Alisema, ili kuhakikisha mitihani haivuji, pamoja na mikakati mingine, pia kuna chumba maalumu (Strong room) kwa ajili ya kuhifadhia mitihani baada ya kutungwa, akisema kiko chini ya ulinzi usiopepesa.
Alisema ingawa chuo hicho ni taasisi binafsi inayofanya biashara, lakini kipaumbele chao ni kutoa huduma bora zisizo za kubabaisha, haki na uadilifu, ili kukijengea hadhi kiendelee kuaminiwa.
Alisema ili wanafunzi waweze kujifunza vizuri na kwa utulivu, chuo hicho kina mahitaji yote ya msingi ikiwemo maabara na vifaa, maktaba na chumba cha kompyuta ambavyo wako huru kutumia.
Kwa upande mwengine, alisema wanaendelea na ujenzi wa jengo jipya la ghorofa sita ili kuongeza madarasa yatakayoweza kubeba wanafunzi wengi zaidi na kuongeza fani nyengine za taaluma hapo baadae.
Alizishauri taasisi na vyuo vyengine vya kiafya, kutumia vyema fursa inayotolewa na serikali chini ya Rais Dk. Hussein Mwinyi, kufanya uwekezaji wenye tija, utakaowanufaisha wananchi na taifa kwa jumla, na si kutazama faida pekee.
Ofisa ubora wa chuo hicho Ibrahim Assad Yussuf, alisema kutokana na jitihada za walimu, shughuli za ufundishaji zinakwenda vyema, kwani hakuna msongamano madarasani unaoweza kushawishi udanganyifu wakati wa mitihani.
“Hizi taarifa au tetesi za kuwepo mambo ya udanganyifu au ‘vibomu’ katika baadhi ya vyuo tunazisikia, lakini hapa kwetu tumejipanga ili tabia hiyo isipenye, na tangu tulipoanza hakuna kesi kama hizo zilizotokea,” alibainisha.
Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzao, Shufaa Ramadhan Wakati na Sharif Omar Khamis (Ufamasia mwaka wa pili), walisema wamechagua kusomea fani hiyo kwa lengo la kuisaidia jamii.
Aidha walisema wanapata matumaini kwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na maduka ya dawa yanayofunguliwa kila uchao, kuajiri vijana wengi, wakijua serikali haiwezi kutoa ajira kwa kila mtu.
Waliwashauri vijana wenzao wanaomaliza kidato cha nne na sita, kuchangamkia fursa za kitaaluma zinazopatikana katika vyuo kama hivyo ili kupata elimu itakayobadilisha maisha yao na kusaidia wananchi.