NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
……..
Wadau wa maendeleo nchini wametakiwa kutembelea maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ili kujifunza na kuona teknolojia mbalimbali katika sekta ya madini na kilimo jinsi zinavyofanya kazi jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi.
Akizungumza katika tamasha la siku maalum ya Iran ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa nchi mbalimbali kujitangaza katika maonesho ya Sabasaba, Mkurugenzi Mtendaji Tanzania Chember Of Commerce Industry and Agriculture(TCCIA) Bw. Oscar Kisanga amesema kuwa ili ufanikiwe katika biashara unapaswa kujifunza kwa watu waliofanikiwa.
Bw. Kisanga amesema kuwa biashara ya sasa inahitaji teknolojia kwani amekuwa akifatilia Japan Day, Korea Day, China Day wamekuwa wakitumia teknolojia na kufanya vizuri.
“Tangu maonesho yaanze nimekuwa nikifatilia siku hizi maalum za nchi mbalimbali na kugundua kuwa biashara zinahitaji teknolojia ili upige hatua kwani ni jambo la muhimu ambalo Watanzania wanapaswa kubadilishana ujuzi na ufahamu na watu wa nchi hizo.” amesema Bw. Kisanga.
Amefafanua kuwa siku ya Iran wameipokea kwa mikono miwili huku akieleza kuwa TCCIA wameona fursa nyingi kutoka kwa nchi hiyo ikiwemo kilimo na kwenye mambo ya madawa.
Amesema kuwa Iran wapo vizuri katika masuala ya utafiti na maendeleo hasa katika dawa za kilimo, huku akitoa wito kwa watanzania kushirikiana na wafanyabiashara kutoka nchi hiyo ili kuangalia namna gani watafanya kazi pamoja.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) Latifa Khamis, amesema kuwa wamejifunza mambo mengi kutoka kwa wafanyabiasahara wa Iran ikiwemo katika madawa ya kupambana na sumu za viumbe hatari kama vile nyoka, ng’e na viumbe wengine hatari.
“Leo ni siku nzuri kwa sababu nchi hizi mbili zimeonyeaha Ushirikiano wa kibiashara na kupelekea wafanyabiashara kunufaika kwa kuwa bidhaa ambazo zinatoka Tanzania zinapelekwa Iran na za Iran zinaletwa Tanzania hivyo kuleta tija katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizi mbili” amesema
Katika tamasha hilo kampuni kubwa za Iran wanaotengeneza chanjo kubwa kubwa wanatafuta washirika nchini Tanzania ili kuhakikisha teknolojia inakuja nchini na kuleta tija kwa Taifa.