Na Sophia Kingimali.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Ajira Vijana na Wenye ulemavu Deogratius Ndejembi ameitaka Mamlaka ya usalama na Afya mahali pa kazi OSHA kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA ili mifumo yao isomane waweze kutambua kampuni na wawekezaji ambao wamekuja nchini ili waweze kuwatambua na kuwafikia kwa wakati.
Hayo ameyasema Julai 7,2024 Jijini Dar es Salaam kwenye maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa wakati alipotembelea banda la OSHA na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo ikiwemo upimaji wa Afya.
Amesema mifumo hiyo ikisomana itamsaidia OSHA kumtambua muwekezaji alipo na kumpa huduma kwa wakati.
“Hii mifumo ikisomana muwekezaji akija akasajili biashara yake hapa akafungua kampuni hapa itakuwa rahisi kumfikia na kumuhudumia kwa haraka”,Amesema.
Aidha amewapongeza OSHA kwa kutumia TEHAMA kwani wamekuwa wakifanyakazi kwa ufanisi kwani taasisi hiyo ni muhimu na inatija kwa maslahi ya Taifa.
Sambamba na hayo amewataka osha kuondoa mfumo wa uaskari pindi wanapotekeleza majikumu yao badala yake watumie zaidi mazungumzo katika kuongea na waajili.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya usalama na Afya mahala pa kazi osha Khadija Mwenda amesema maagizo na ushauri uliotolewa na waziri watakahikisha wanaufanyia kazi kwani kwa sasa wamejipanga vizuri katika kutoa huduma kwa kuwa wamewekeza kwenye vItendea kazi vya kisasa na matumizi ya TEHAMA.
Amesema mpaka sasa wameshasajili sehemu za kazi 45000 ambazo wanazipitia mara kwa mara na kuzishauri huku zoezi la kusajili likiwa linaendelea.
Adha ametoa rai kwa wananchi kufika kwenye banda lao ili kupata elimu ya shughuli zao wanazofanya lakini kupata huduma ya upimaji afya bure.
“Mpaka sasa tangu sabasaba imeanza tumeshawapima afya watu zaidi ya 300 lakini pia tumekuwa sehemu ya majibu kwa maswali ambayo wadau wamekuwa wakijiuliza”,Amesema.