Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akikaribishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis mara baada ya kuwasili rasmi Ofisi hiyo katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 08 Julai, 2024.
………
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Ofisi hiyo itaendelea kusimamia maono ya viongozi wakuu wa Serikali katika kuimarisha usimamizi wa mazingira na kudumisha Muungano.
Dkt. Kijaji amesema hayo leo tarehe 08 Julai, 2024 wakati wa makabidhiano ya Ofisi hiyo baina yake na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo yaliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Amesema mtangulizi wake (Dkt. Jafo) amefanya kazi kubwa na nzuri iliyoacha alama na kwa kuzingatia umuhimu huo ataendeleza juhudi hizo ili kuhakikisha sekta za Muungano na Mazingira zinaleta matokeo na malengo tarajiwa kama inayoelekezwa na Viongozi Wakuu.
“Naahidi ushirikiano na Menejimenti na nitaendelea kujifunza masuala yote yanayoihusu Ofisi hii kwa kushirikiana na wenzangu na kuhakikisha pale ulipoishia tunaendelea napo kwa kasi zaidi ili kufikia malengo yaliyowekwa” alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa Ofisi wezeshi kutokana na majukumu yake kugusa maisha ya kila siku ya jamii na hivyo atakuwa mtumishi wa wananchi na kuwa tayari kujitoa ili kuhakikisha kunakuwa na Tanzania yenye Muungano imara, Mazingira safi, salama na endelevu.
Alisema katika kutimiza adhma ya Viongozi Wakuu wa Serikali, Dkt. Kijaji aliahidi kufanya kazi kwa karibu zaidi na Menejimenti ya Ofisi hiyo ili na kuunganisha nguvu ya pamoja ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sekta za Muungano na Mazingira.
Alifafanua kuwa ajenda Muungano na uhifadhi wa mazingira kwa sasa ipo masikio mwa Watanzania walio wengi kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Viongozi na watendaji wa Ofisi hiyo, wajibu ambao amejipanga kuhakikisha anausimamia kwa nguvu zote kuutekeleza.
Awali Waziri akikabidhi ofisi, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo amemhakikishia Dkt. Kijaji ushirikiano na kumweleza kuwa menejimenti ya ofisi hiyo imejaa watalaamu wenye weledi katika kusimamia majukumu katika yao ya kazi.
“Nikuhakikishie Ofisi hii imejaa wasomi wa kutosha wenye uzoefu na weledi wa hali ya juu…Nilipewa ushirikiano wa kutosha ambao uliniwezesha kutekeleza majukumu yangu ni imani yangu kuwa ushirikiano huu utazidi kuimarika,” alisema Dkt. Jafo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amemweleza Dkt. Kijaji viongozi na Watendaji wa Ofisi hiyo wapo tayari kufanya kazi kwa muda wote ili kuhakikisha sekta ya Muungano na Mazingira zinaleta tija iliyokusudiwa.
“Ofisi hi ina bahati ya kuwa na wataalamu wa masuala ya mazingira, vyanzo vya maji na wataalamu wa miti ambao wanatoa ushauri kuhusu kipindi kipi ni kizuri na sahihi kwa ajili ya upandaji” alisema Mhe. Khamis.
Aidha Naibu Waziri Khamis ameshukuru Waziri Jafo kwa kusimamia vyema ofisi ya Makamu wa Rais katika kipindi chote alichohudumu Ofisi hiyo kwani alikuwa mwalimu kwa viongozi na watendaji katika kutekeleza majuk