Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuona fursa mbalimbali za uwekezaji zinatopatikana kupitia nchi 26 zilizoshiriki maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam(DITF) hususan Japan.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TANTRADE), Latifa Hamis katika mkutano maalumu wa wa wafanyabiashara wa Tanzania na Japan.
Alisema lengo la mkutano huo ni kutafuta fursa za wafanyabiashara wa Japan kuwekeza nchini huku wafanyabiashara wanchi hiyo wakionesha bidhaa mbalimbali kama kompyuta, simu na magari.
“Mkutano huo umehudhuriwa na kampuni tisa katika sekta mbalimbali kama uvuvi, afya, teknolojia, kilimo na usafirishaji ambazo zimekuwa zikionesha fursa za uwekezaji zilizopo,” alisema.“ Ninawataka Watanzania wajitokeze kwa wingi katika maonesho hayo kwa kuangalia fursa mbalimbali zinazotolewa na nchi zilizoshiriki maonesho kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali,” alisema.
Kwa upande wake balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa alisema amevutiwa na maonesho hayo kwani yanawapa fursa ya kujifunza vitu vingi kutoka Tanzania.