Vijana wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao kuhusu huduma za fedha katika mamlaka husika ili kupata suluhu haraka pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Fedha ikiwemo utapeli, udanganyifu na mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza/ kausha damu).
Mamlaka wanazotakiwa kuwasilisha malalamiko hayo ni Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Dhamana ya Masoko na Mitaji, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wito huo umetolewa Ikungi mkoani Singida na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, baada ya kutoa elimu ya fedha katika Kongamano la Vijana wa Wilaya hiyo katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru.
Bi. Mjema alisema Serikali imeweka kanuni na miongozo ili malalamiko hayo yaweze kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Sheria za Fedha.
“Waende Benki Kuu kama malalamiko yao yanahusu masuala ya benki, kama yanahusu masuala ya dhamana ya masoko na mitaji basi waende Mamlaka ya Dhamana ya Masoko na Mitaji, kama yanahusu bima yapelekwe Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na yale yote yanahusiana na mafao ya uzeeni waende Ofisi ya Waziri Mkuu”, alifafanua Bi. Mjema.
Alisema katika Kongamano hilo Wizara ya Fedha imetoa elimu ya fedha kwa vijana kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, elimu ya mikopo, uwekaji wa akiba, uwekezaji, maisha baada ya kustaafu, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha na namna ambavyo Serikali imeweka miongozo mbalimbali ya kumlinda mtumiaji wa huduma ndogo za fedha kupitia Kanuni za Kumlinda Mtumiaji.
“Tumewaelimisha vijana kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha ikiwemo kuwekeza katika Masoko ya Mitaji, mifuko ya uwekezaji wa pamoja, upatikanaji wa mikopo katika benki na taasisi za fedha pamoja na huduma ndogo za fedha”, alibainisha Bi. Mjema.
Alisema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwawezesha wananchi hususan vijana kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya fedha ili waweze kujenga uchumi wao, wa familia na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Naye Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Peter Musa alisema wameona ni vema kuialika Wizara ya Fedha kutoa elimu ya Fedha kwa kuwa kwa sasa masuala ya fedha yamekuwa changamoto hususan kwa vijana.
Alisema pamoja na kuwa Wizara imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kusambaza elimu hiyo nchini lakini waliona mkusanyiko wa Jukwaa la Vijana katika shughuli za Mwenge ni sehemu muafaka kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.
Kwa upande wa vijana walioshiri Kongamano hilo, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa elimu hiyo muhimu kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Bw. Rajabu Kulandera miongoni mwa washiriki ambaye alisema kutokuelewa vizuri sekta ya fedha kumekuwa kukiwakosesha haki wananchi wengi hususan vijana ambao mara nyingi wanajiona kuwa kundi lililosahaulika lakini baada ya elimu hiyo ameelewa haki na wajibu wao kama watumiaji wa huduma za fedha , umuhimu wa kuweka akiba, kutumia mifumo rasmi ya fedha pamoja na namna ya kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.
“Elimu hii imetufumbua macho, pamoja na mambo mengine suala la mikopo ni kaa la moto kwetu, lakini baada ya elimu hii tumeelewa umuhimu wa kusoma mikataba kabla ya kukopa ili kujua kama mkopo ni kausha damu au ni wa afya”, alisema Bw. Kulandera.
Aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuendelea kutoa elimu muhimu kwa wananchi wa hali ya chini hususani vijijini ili kuwanusuru na mateso wanayoyapata yanayotokana na kutokujua mifumo rasmi pamoja na haki zao hali inayowafanya waangukie katika kuchukua mikopo holela yenye masharti magumu.