Na Sophia kingimali.
WATANZANIA wanaotaka kusoma nje ya nchi wametahadharishwa kuwa makini kwa kuangalia taasisi wanazokwenda kusoma kuwa zinatambuliwa na mabaraza ya mtihani ya nchi husika.
Kauli hiyo imekuja baada ya kubainika kuwepo na changamoto ya baadhi ya wanafunzi wa kitanzania kushindwa kufanyiwa ulinganifu wa matokeo ya mtihani na Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA) kutokana na chuo alichosoma kutotambuliwa.
Akizungumza Julai 7,2024 mara baada ya kutembelea banda la Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam(DIFT), Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed amesema wamekuwa wakitoa huduma ya ulinganifu wa matokeo ya mitihani kwa wanafunzi waliosoma nje ya nchi lakini imekuwa changamoto kwa baadhi kusoma kwa vyuo visivyotambuliwa na mabaraza la mitihani.
“Kuna watanzania wanasoma nje wanarudi kwa lengo la kujiendeleza vyuo vikuu hapa nchini inabidi tuwafanyie ulinganifu wa matokeo ya mtihani ili cheti cha nje kiendane na cheti chetu cha ndani, katika eneo hilo changamoto tunayokutana nayo ni kubwa.
“Watu wanapokwenda kusoma nje waangalie taasisi wanazokwenda kusoma zinatambuliwa na mabaraza ya mitihani ya kule, NECTA inafanya ulinganifu wa matokeo, vyeti vinavyotolewa na baraza la mitihani kwa mfano mtu amesoma Lesotho akirudi Tanzania ili tufanye ulinganifu tunaangalia cheti kilichotolewa na baraza la mitihani cha nchi ile kama amesoma katika taasisi ambayo haijasajiliwa akirudi hatuwezi kumfanyia,” amesema.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa wazazi kuhakiki majina ya watoto wao wanapowasajili shule yaendane kwa mujibu wa Cheti cha kuzaliwa kwa sababu sasa hivi wanapata changamoto ya wanaoomba vyeti mbadala kukataliwa kwa kukosea jina.
Katibu hiyo amesema mtoto akishafanya mtihani wa darasa la nne kubadili jina inakuwa ni changamoto hivyo wahakiki majina yao wakati wa usajili hadi darasa la tatu.
Aidha baraza linawakaribisha wananchi katika banda lao ili kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na baraza hilo ikiwemo utoaji wa vyeti ambapo kwa sasa huduma hiyo inapatikana kwenye maonesho hayo.
“Hapa tunatoa huduma ya cheti mbadala kwa wale wote waliopoteza vyeti akija na viambatanisha ikiwemo kitambulisho cha urai/nida/leseni au passport,barua ya polisi atasaidiwa hapa hapa na atapata cheti chake”,Amesema.