Mwinjilisti wa Kimataifa kutoka Taasisi inayojihusisha na kazi ya kuokoa Roho za watu ya (SOS) Johanes Amrtizer, Askofu wa Kanisa la TAG Jimbo la Pwani na Dar es Salaam Uswege Mwakisyala, Katibu wa Kamati Maandalizi ya Mlipuko wa Furaha Festival Mchungaji Timothy Mwita pamoja na waimbaji wa nyimbo za injili wakizungumza na waandishi wa habari leo Julai 8, 2024, Dar es Salaam.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katika kuelekea kilele Cha Maadhimisho ya miaka 75 ya Kanisa la TAG, Kanisa hilo kwa kushirikiana na Taasisi inayojihusisha na kazi ya kuokoa Roho za watu ya (SOS) wameandaa Tamasha la Mlipuko wa Furaha ‘FURAHA FESTIVAL’ ambalo limelenga kuwaombea na kuwaponywa watu wenye changamoto mbalimbali nchini.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Mwembe Yanga uliopo Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam kuanzia Julai 9, 2024 hadi Julai 13 mwaka huu ambapo waimbaji mbalimbali wa nyimbo za injili watashiriki kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Rose Muhando, Boaz Danken, Miriam Lukindo Mauki pamoja na Julia Willkander.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 8, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwinjilisti wa Kimataifa kutoka SOS Johanes Amrtizer ambaye ni Muhubiri Mkuu katika tamasha hilo, amesema kuwa pamoja na kuokoa makundi ya watu pia watatumia tamasha hilo kufundisha na kukemea vitendo vya rushwa, imani potofu za kishirikina ambazo zinapelekea mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mwinjilist Amrtizer amesema kuwa lengo ni kuhakikisha watu kunakuwa huru kutoka katika magonjwa na kuleta furaha kwa wasio na matumaini kama Mwenyezi Mungu alivyokusudia.
‘Kutakuwa na timu mbalimbali za wainjilisti zitakazo toa huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam katika kipindi chote cha tamasha ambalo litaanza saa kuanzia saa tisa alasiri” amesema Mwinjilist Amrtizer.
Mwinjilisti amesema kuwa katika tamasha hilo kutakuwa na semina zitakazotolewa katika uwanja wa uhuru kwa vijana pamoja na kufanya maombi ya kuwaombea viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa hekima, maarifa na busara katika kuliongoza Taifa.
Amefafanua kuwa katika tamasha hilo kutakuwa na timu ya watu 250 kutoka nchi tofauti tofauti ambao wataungana na wakazi wa Dar es Salaam kuhubiri upendo wenye nguvu ya Yesu Kristo.
Aidha amesema kabla ya tamasha hilo wamefanikiwa kuutana makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara kwa ajili ya kuwashauri namna ya kukua kiuchumi pamoja na kutembelea vituo vya watu wenye uhitaji.
Askofu wa Kanisa la TAG Jimbo la Pwani na Dar es salaam Uswege Mwakisyala, amesema kilele Cha Maadhimisho hayo kinafanyika katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam Julai 14 mwaka huu.
Askofu Mwakisyala amesema kuwa mkutano huo utashirikisha wamisionari zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali ambao utapambwa na nyimbo za kumtukuza Mungu kutoka kwa waimbaji mbalimbali.