Waziri wa nchi ofisi ya Rais uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo akizungumza katika uzinduzi huo mkoani Arusha.
Washiriki kutoka taasisi na makampuni mbalimbali wakishuhudia uzinduzi huo mkoani Arusha
………………
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Uwekezaji,Profesa Kitila Mkumbo,amesema mwelekeo wa Serikali ni kuondoa utitiri wa leseni za biashara ambapo mwekezaji yeyote hata kama ana miradi mingi atakuwa na leseni moja tu.
Mkumbo,ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizindua Kituo cha uwekezaji,TIC , Kanda ya kaskazini kwenye Ukumbi wa makao makuu ya jengo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,NCAA,Jijini Arusha.
Amesema kuwa kituo hicho kitakuwa ni cha Kanda ya kasikazini ambapo makao makuu yanahama Kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro na kuhamia Arusha ambapo kuna shughuli nyingi za uwekezaji ukilinganisha na mikoa mingine lengo ni kuimarisha uratibu wa shughuli za uwekezaji .
Amewataka wafanyabiashara na wasomi kuchangamkia masoko ya nje kutokana na fursa zilizopo ili kupata ajira na kufanya biashara badala ya kung’ang’ania Soko la ndani pekee.
“nchi yetu imezungukwa na nchi nyingi ambazo hazina bandari na wafanyabiashara katika nchi hizo wanategemea bandari yetu, hivyo wafanyabiashara wa hapa nchini wachangamkie fursa za kufanya biashara kwenye masoko ya nje sanjari na wasomi mbalimbali ili nao wachangamkie fursa za ajira nje ya nchi ambazo ni nyingi.”amesema .
Ameongeza kuwa, Serikali imewekeza sana kwenye miundo mbinu ili kurahisisha usafirishaji na usafiri hivyo barabara hizo hazijengwi kwa mapambo bali kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka eneo moja kwenda lingine na nchi yetu inaongoza kwa kuwa na barabara nzuri kwa nchi za Afrika.
Amefafanua kuwa, vipaumbele vya Serikali ni kuongeza tija katika kilimo ambacho utoshelevu wa mazao ni asilimia 124% ambacho kinaweza kuhudumia Wananchi kwa miezi minne mfululizo ikiwa kama kutatokea changamoto yeyote.
Aidha ametaja kipaumbele kingine ni kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo pamba na kuyaongezea thamani na kuyauza nje kwa thamani kubwa,kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyauza.
Hata hivyo amelitaka Shirika la Viwango Nchini (TBS) kuwasaidia wafanyabiashara badala ya kugeuka kuwa kamata kamata kwani wafanyabiashara wanahitaji kusaidiwa ili kukuza mitaji yao waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyotakiwa na kupata masoko ya ndani na nje .
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Arusha Paulo Makonda amesema kuwa kituo hicho cha uwekezaji kilichozinduliwa Arusha kitakuwa ni cha mfano kwa Afrika na kitakuwa na watendaji wenye maamuzi na uwezo na makini na hivyo hakutakuwepo ucheleweshaji pindi mwekezaji anapifika kwa ajili ya kutumia fursa zilizopo.
Amesema Mkoa umetenga hekari 6837.46 kwa ajili ya Uwekezaji kwenye shughuli za kilimo.
Ameongeza kuwa, katika robo ya mwaka, Arusha ni namba moja katika Utalii ambapo katika robo ya mwaka imekuwa ni ya tano duniani
Naye Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha uwekezaji nchini ,Gilead Teri,amesema kuhamishiwa makao makuu ya Kituo hicho kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro hadi Arusha,ni kutokana na wingi wa shughuli za uwekezaji .
Amesema kuwa uzinduzi wa Kituo hicho ni kutokana na maelekezo ya maadhimio ya kongamano la Utalii lililofanyika mwezi Aprili mwaka huu Jijini Arusha,na kuagiza kufunguliwa Kituo cha uwekezaji mkoani Arusha ili kurahisisha huduma kutokana na mkoa wa Arusha kuwa na fursa na maeneo mengi uwekezaji ikiwemo,Utalii,madini na kilimo tofauti na mikoa mingine ya kaskazini .
Amesema mwaka 2023 Kituo hicho kilisajili miradi 526 yenye thamani ya Dola milioni 5.92 za kimarekani na mwaka 2024 juma ya miradi itakayosajiliwa ni 826 yenye thamani ya Dola milioni 405.
Teri amesema kuwa ,kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu jumla ya miradi iliyokwisha sajiliwa ni 405 yenye thamani ya Dola bilioni 2 huku lengo ni kusajili miradi 800 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu .