Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali ya Tanzania yameivutia kampuni maarufu ya teknolojia ya China, Shanghai Sixunited Technology Company Limited kuja kuwekeza nchini.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Kanda wa Maendeleo ya Biashara, Theresia Mwita wakati wa uzinduzi wa bidhaa mpya za kisasa za Acer Gadget (e10) kwenye hotel ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam Ijumaa Julai 5, 2024.
Theresia alisema kuwa Tanzania imeweka mazingira rafiki katika uwekezaji jambo ambalo limewafanya wao kuja kuwekeza na kupanua wigo wa biashara.
“Uwekezaji wetu utakwenda sambamba na ongezeko la soko la ajira kwa watanzania ambapo watafanya Bashara na sisi huku tukirahisisha uendaji kazi katika sekta mbalimbali. Kampuni yetu inazalisha bidhaa za kisasa kama hii ya Acer Gadget (e10) ambayo ina wigo mpana katika matumizi. Inatumika katika sekta ya elimu, biashara na nyinginez,” alisema Theresia.
Alisema kuwa Acer Gadget (e10) imetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu kwa kuzingatia maendeleo ya kidigitali katika sekta tofauti duniani.
Kwa mujibu wa Theresia, tangu kuanzishwa kwa kampuni mwaka 2015 mjini, Shanghai, China, Sixunited imeweza kutoa huduma za suluhisho la moja kwa moja kwa bidhaa za kielektroniki kwa watumiaji wake na vile vile kwa bidhaa za mtandao wa akili au intelligent software.
‘Kampuni yetu imebobea katika utengenezaji na huduma za uendeshaji za bidhaa za programu na vifaa vya akili (Intelligence) na nyinginezo nyingi za kieletroniki.
Alifafanua kuwa bidhaa zao zinajumuisha Kompyuta za mkononi, tableti, mini PC, AIO, vifaa vya PC, seva, IoT, Udhibiti wa Viwanda nyinginezo.
Alisema kuwa kampuni yao imekuwa ikijitolea kukuza uvumbuzi wa bidhaa za kiteknolojia duniani na mabadiliko yake kidigitali.
“Hivi sasa, Sixunited ina wafanyakazi zaidi ya 1,100, ambapo zaidi ya asilimia 60 ni wafanyakazi wa waliobobea katika masuala ya maendeleo ya utafiki, uchumi wa viwanda, mauzo na huduma. ”alisema.