Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Tanzania NHC , Hamad Abdalla akitembelea banda la NHC wakati alipotembelea maonesho ya Sabasaba yanayoendelea barabara ya Kilwa Julai 5, 2024 jijini Dar es Salaam, Kulia ni Muungano Saguya Meneja Mawasiliano na uhusiano wa shirika hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Tanzania NHC , Hamad Abdalla akipata maelezo Katika banda la NHC wakati alipotembelea maonesho ya Sabasaba yanayoendelea barabara ya Kilwa Julai 5, 2024 jijini Dar es Salaam, Kulia ni Muungano Saguya Meneja Mawasiliano na uhusiano wa shirika hilo.
………………
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Tanzania NHC , Hamad Abdalla amewataka watanzania kujiandaa na awamu ya pili ya mradi wa Samia Housing Scheme -Kawe baada ya miezi mitatu ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari ,kwenye maonesho ya biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayoendelea barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, ameeleza awamu ya kwanza ya mradi huo, Samia Housing Scheme wenye nyumba 560 wamemaliza kuuza.
Alielezea, nyumba hizo zimegharimu zaidi ya sh.bilioni 48.2 eneo la Kawe ambapo wanachofanya kwa kwasasa ni kupata maoni ya watanzania .
“Nimepata fursa ya kutembelea banda letu, niwasihi wananchi wafike kujionea bidhaa tunazozinadi,kuna miradi ambayo tumekuja nayo”
Hamad alieleza, kati ya miradi ambayo wataweza kupata ufafanuzi wake ni pamoja na ule wa seven eleven (711) Kawe, mradi ambao ulikwama kwa muda mrefu.
“Tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuliwezesha Shirika kutupa ruksa ya kuendelea kuchukua fedha kwenye Taasisi za kifedha ,na kuweza kurejea site na mradi unaenda Kwa Kasi sana na sasa tupo ghorofa ya 12 na tayari mauzo yameanza,
“Na tunatumia fursa hii ya viwanja vya sabasaba kwa ajili ya kuuza mradi huu wa 711;”
Hamad alifafanua kwamba, mradi mwingine ni ule wa Morocco Square ambao nao unaenda vizuri.
Vilevile,Kuna miradi mipya wameanza, kama pale Kashozi Commercial Complex -Bukoba ambao ni mradi wa jengo la biashara.
Kuna mradi wa Masasi,mradi wa maduka na maeneo ya biashara na maofisi.
Alitaja miradi mingine kuwa ni sanjali na mradi wa Mtanda huko Lindi , Mradi wa Mtoni Kijichi -Temeke ambao huu ni Samia Housing Scheme.
Hamad alibainisha, Kahama kuna maduka ambayo wanajenga eneo la stand ya mabus Kahama.
Mkurugenzi huyo anasema, licha ya miradi yote hiyo ambayo wanajenga na kuuza,ama kujenga na kupangisha pia wana huduma ya wale watanzania wanaotaka miradi ya ubia.
“Wiki moja iliyopita tumetangaza miradi ya ubia katika maeneo mbalimbali ya Tanzania hivyo tunaomba wanaotaka waje kwenye banda letu kujua kuhusu sera inasemaje na ufafanuzi zaidi”
Hamad aliwatoa hofu watanzania, kuhusu gharama za Nyumba na kusema, utoaji huduma umefikia wananchi wa hali ya chini, hali ya kati.
“Mfano ni pale kwenye mradi wa Samia Housing Scheme utaona ni magorofa 560 tuliowakusudia ni wenye kipato cha kati kuna nyumba kuanzia gharam ya milioni 50 , ambapo wanaoanza maisha imekuwa ni kimbilio kwao” anaeleza Hamad.