* Wajadili kinagaubaga kuhusu nafasi ya watu wenye ulemavu katika Taasisi za Umma.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Mabula Misungwi Nyanda amekutana na Mkurugenzi wa Taasisi ya watu wenye ulemavu ( Foundation for Disabilities Hope – FDH) Bw. Michael Salali na kufanya mazungumzo kuhusu nafasi ya Taasisi za Umma katika kuhudumia na kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za uhifadhi na utalii.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro Julai 04, 2024 yalijikita katika kuangalia namna Taasisi za Umma zinavyoweza kutoa huduma rafiki kwa watu wenye ulemavu mfano lugha za alama (sign language) kwa viziwi, kuangalia utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa TAWA ili waweze kuwahudumia makundi ya watu wenye mahitaji maalum kuhusu namna ya kupata vibali na kutembelea maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwa lengo la kutalii.
Kupitia mazungumzo hayo, Bw. Michael Silali alimwomba Kamishna wa Uhifadhi-TAWA kuangalia uwezekano wa taasisi hizo (TAWA na FDH) kushirikiana katika masuala mbalimbali yatakayoweza kuhusisha vijana wenye ulemavu katika fursa za kukuza uchumi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Bw. Michael alilitaja Shirika la madini STAMICO kuwa miongoni mwa Mashirika ambayo yameimarisha mashirikiano na Taasisi anayoiongoza (FDH) ambapo wamefanikiwa kubadili makaa ya mawe kuwa mkaa ambao matumizi yake ni rafiki kwa wenye ulemavu wa ngozi.
Kwa upande wake Kamishna Mabula alimshukuru Mkurugenzi huyo kwa kutembelea ofisi za TAWA na kwamba anatambua kuwa moja vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha watu wenye ulemavu na kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na maendeleo ya Taifa. Hivyo, alimweleza kuwa amepokea ombi lake kwa mikono miwili na atalifanyia kazi ipasavyo.