RAIS Mstafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amewapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusambaza nishati ya umeme kwa vijijiji 12,031 na kuongeza kuwa wakati akiwa anaondoka madarakani mwaka 2015 umeme ulikuwa umefika kwenye vijiji 2,000 tu.
Dkt. Kikwete ametoa pongezi hizo jioni ya leo Tarehe 6 Julai, 2024 alipotembelea banda la REA kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF); yanayoendelea katika viwanja vya Saba Saba, barabara ya Kilwa, Jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu Kikwete amepongeza kazi kubwa ya kusambaza nishati ya umeme vijijini na kusema wakati anaingia madarakani mwaka 2005 ni asilimia 4 tu ya Wananchi wa vijijini ndio walikuwa wamefikiwa na nishati ya umeme.
“Leo zaidi ya vijiji 12,031 vimeunganishwa na umeme, ni zaidi ya asilimia 98, vilivyobaki ni vijijini 207 tu,”. Alisema Dkt. Kikwete.
Amesema kwa idadi hiyo ni wazi kuwa Wananchi wengi wa vijijini wameunganishwa na umeme na hivyo kufanya watumiaji wa umeme nchini kuongezeka na kuwa iwapo bei ya umeme itapungua, itawafanya Wananchi wengi zaidi kutumia nishati hiyo kwa kupikia kwa sababu kuna majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo.
“Tuangalie TANESCO wasipandishe bei ya umeme; Wananchi wengi wataweza kuutumia umeme kama nishati safi ya kupikia, sasa hivi mkaa na kuni ndio wapinzani wakubwa wa umeme. Miti inakatwa kweli kweli, tunaharibu mazingira, na hatupandi miti kwa kasi ile ile,”. Amesema Dkt. Kikwete.
Ametoa mfano kuwa miaka kadhaa iliyopita akiwa nyumbani kwake Msoga, mkoani Pwani alikuwa hawezi kuona hata magari yakipita Chalinze kwa sababu ya misitu ya miti, lakini sasa anaweza hata kuhesabu idadi ya magari yanayopita Chalinze akiwa Msoga na kuwa misitu imebaki tu kwenye makaburi.
“Matumizi ya mkaa ni makubwa, miti inakatwa sana, tupunguze matumizi ya mkaa na kuni lakini pia tupande miti na tutumie nishati safi yakiwemo majiko banifu, lakini bei ya umeme iangaliwe na ipungue ili Wananchi wengi waitumie.” Alisisitiza Rais Mstaafu, Dkt. Kikwete.
Dkt. Kikwete ametoa wito kwa wauzaji wa gesi ya kupikia wasiwe na tamaa kupandisha bei ili Wananchi wengi wahamasike kuitumia katika kupikia.
Amesema nishati ya umeme si kwa ajili ya kupikia tu na ikiwa itawafikia Wananchi wengi wataitumia katika shughuli za uzalishaji mali na kuboresha maisha yao kuichumi.
Kuhusu ubora wa bidhaa na Waoneshaji kwa ujumla wakati wa maonesho ya Saba Saba; Dkt. Kikwete alisema umeendelea kuwa bora ukilinganisha na miaka iliyopita lakini pia hata Waoneshaji wanaoelezea bidhaa na huduma, wanatoa maelezo kwa ufasaha na yanayojitosheleza.