Leo Julai 6, 2024, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ Bank) imetoa gawio la Shilingi Bilioni Saba (TZS 7 Billion) kwa mwanahisa wake pekee, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Makabidhiano ya Gawio hilo yalifanyika kwenye Mkutano wa Mwaka wa Wanahisa (AGM) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano, Makao Makuu ya PBZ, Mpirani, Zanzibar.
Akipokea kwa niaba ya serikali, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais; Fedha na Mipango; Mhe. Dr. Saada Mkuya Salum, ameipongeza PBZ Bank kwa mafanikio inayoendelea kuyapata na kutaka benki iendelee na utendaji wake kwa ufanisi na uweledi.
Makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Mkurugenzi Muendeshaji wa PBZ Bank, Ndg. Arafat A. Haji, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Ndg. Joseph Meza, Wakurugenzi wa Bodi ya PBZ Bank na baadhi wa viongozi wa Menejmenti ya PBZ Bank. Aidha kwa upande wa Mwanahisa, Gawio lilipokelewa na Mhe. Dr. Saada Mkuya Salum, wakishuhudia alikuwepo Katibu Mkuu, Afisi ya Rais; Fedha na Mipango, Mhe. Dr. Juma Akil Malik, Pamoja na Msajili wa Hazina, Mhe. Waheed Sanya.
Ndani ya Mwaka 2023, PBZ Bank ilifanikiwa kukuza faida yake hadi kufikia Shilingi Bilioni 74 faida kabla kodi na Rasilimali kufikia Shilingi Trilioni 2.05.
PBZ Bank imeendelea kutanua huduma zake kwenye mikoa mengine ya Tanzania Bara kwa kufungua matawi Morogoro na Mbeya.