Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga (kushoto) akiwa na Tawfik Jelassi, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) hivi karibuni jijini Paris, Ufaransa. UNESCO imetangaza utayari wake wa kuiunga mkono Tanzania katika juhudi za kuimarisha juhudi za kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini. (Picha kwa hisani ya Tume ya TEHAMA).
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga (kushoto) akiwasilisha mada katika moja ya vikao kazi vilivyofanyika jijini Paris, Ufaransa hivi karibuni. Kulia ni Tawfik Jelassi, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo limetangaza utayari wake wa kuiunga mkono Tanzania katika juhudi za kuimarisha juhudi za kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini. (Picha kwahisani ya Tume ya TEHAMA)
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo limetangaza utayari wake wa kuiunga mkono Tanzania katika juhudi za kuimarisha juhudi za kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini. Utayari huo umekuja baada ya Mkurugenzi huyo kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga hivi karibuni jijini Paris, Ufaransa. (Picha kwa hisani ya Tume ya TEHAMA).
………………………..
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetangaza utayari wake wa kuiunga mkono Tanzania katika juhudi za kuimarisha juhudi za kuleta mabadiliko ya kidijitali nchini.
Hayo yamesemwa na Tawfik Jelassi, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari na Mawasiliano wa UNESCO yenye makao yake makuu jijini Paris, Ufaransa katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Tume ya TEHAMA nchini, Dkt. Nkundwe Mwasaga ambaye hivi karibuni alikuwa nchini humo kikazi.
Alisema UNESCO imeguswa na kasi na utayari wa Tanzania katika mchakato wake wa kupambana kuyafikia mapinduzi halisi ya kidigitali na kusisitiza, “Ujuzi wa kidijitali ni nguzo muhimu kwa mafanikio na uendelevu wa mabadiliko ya kidijitali. Tunayo furaha kuunga mkono Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya TEHAMA katika kuboresha ya ujuzi wa kidijitali.”
Aliongeza kuwa, Mfumo wa Umahiri wa UNESCO kwa Umma kuhusu Akili Bandia/Mnemba (AI) na mabadiliko ya Kidijitali umeundwa kama zana hai ya maendeleo, kusaidia nchi wanachama katika mabadiliko yoyote yanayotokea.
“Kutokana na hali hiyo, tunapendekeza kwamba Tume ya TEHAMA ya Tanzania na UNESCO kwa pamoja tuanzishe Utafiti wa Tathmini ya Mahitaji kuhusiana na ujuzi wa kidijitali Serikalini na Umma kwa ujumla, ikifuatiwa na afua za kujenga uwezo ili kushughulikia mapungufu ya umahiri yaliyotambuliwa.
“Mbali ya mambo ya kimsingi ya usimamizi wa data, faragha, usalama wa mtandao na AI, mafunzo kwa maofisa wakuu yatazingatia umahiri zaidi wa kimkakati kama vile ushirikiano, utabiri wa kimkakati na muundo wa huduma ya umma unaozingatia binadamu,” alisema Jelassi aliyempongeza kwa uongozi wake ndani ya Tume ya TEHAMA huku akisisitiza anaamini Tume itachangia mabadiliko ya Tanzania kuwa kitovu cha kimataifa cha uvumbuzi.
“Tunatazamia kufanya kazi na wewe na kuwahakikishia uungaji mkono wetu katika mchakato wa mageuzi ya kidijitali Tanzania,” alisema.
Naye Dkt. Mwasaga akizungumzia utayari wa Tanzania katika kuongeza kasi ya mageuzi ya kidijitali, alisema umewezeshwa na ushirikiano kati ya Tume ya TEHAMA na Ofisi ya UNESCO jijini Dar-es-Salaam chini ya uongozi wa Michel Toto, Mwakilishi wa UNESCO katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.