Na Lucas Raphael, Tabora
VYAMA vya Ushirika nchini vimetakiwa kutunza vizuri na kwa usahihi kumbukumbu za taarifa zao za mapato ili kuepuka kuandikiwa madeni makubwa yasiyolingana na uhalisia wa biashara zao.
Hayo yamebainishwa jana na Wataalamu wa Kampuni ya Alpha Associates Tanzania Ltd katika wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Nane Nane Ipuli Mjini Tabora.
Akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea Banda la Kampuni hiyo ili kujionea shughuli zinazofanyika, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Dkt Alphonce Massaga alisema kuwa vyama vya ushirika vina shida ya utunzaji taarifa ndiyo maana wamekuja kutoa elimu ili kuokoa fedha zao.
Alibainisha kuwa wamealikwa na Tume ya Ushirika ili kuja kutoa elimu ya namna bora ya kuandaa hesabu zao za mwaka na utunzaji sahihi wa kumbukumbu za taarifa hizo ili kuepuka kuandikiwa kodi ya mamilioni na Mamlaka ya Mapato.
Alisisitiza kuwa Vyama vya Ushiriki vilivyo vingi vina changamoto ya kikodi hali ambayo husababishwa na ukosefu wa elimu ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu zao na viambatanisho sahihi vinavyopaswa kuwepo.
Dkt Alphonce alifafanua kuwa kila taasisi inapaswa kujua mapato yake ni kiasi gani kwa mwaka na kuandaa taarifa zao kwa usahihi na nyaraka zinazosapoti taarifa hizo zinapaswa kuonesha uhakisia, kinyume na hapo utadaiwa kodi kubwa.
‘Wito wangu kwa vyama vya ushirika wajitahidi kutunza vizuri na kwa usahihi kumbukumbu zao na watumie nyaraka zinazokubalika kisheria ambazo ni za malipo ya kielektroniki (EFD) na kujiepusha na nyaraka zisizokubalika’, alisema.
Aidha alisisitiza kuwa kwa taasisi kubwa zenye uwezo wa kuingiza sh mil 200 au zaidi kwa mwaka hizi zinatakiwa kuingia kwenye mfumo wa VAT ila baada ya kujiridhisha pasipo shaka kuwa kiwango chao kimepanda tofauti na awali.
Alibainisha malengo makuu ya taasisi hiyo kuwa ni kutoa elimu kwa Mameneja na Wajumbe wa Bodi za vyama ya ushirika na hicho ndicho wamekuja kufanya katika maadhimisho hayo ili kuelimisha viongozi, wanachama na wadau wengine.
Alisema malengo mengine ni kutoa ajira kwa jamii na kusaidia taasisi ikiwemo vyama vya ushirika kuandaa taarifa sahihi za hesabu zao za mwaka ili walipe kodi stahiki na sio kubambikiwa kodi isiyoendana na biashara zao.
Alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya vyama 10 kutoka Mikoa mbalimbali vimepewa elimu hiyo na kuwasaidia kufutwa kwa mabilioni ya fedha za madeni yaliyotokana na kupewa makadirio makubwa.