Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Yamungu Kayandabila akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 4, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa BoT
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema hali ya uchumi imeendelea kuimarika kwa
kumechangiwa kwa kiasi kikubwa ukuaji imara wa mikopo kwa sekta binafsi na utulivu wa sekta ya fedha katika robo ya pili ya 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julia 4, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, amesema Kuwa tathmini mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024
Dkt. Kayandabila amesema kuwa kamati imeamua riba ya benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024 ili kuleta tija katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Maamuzi hayo yamezingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia, ambapo matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani pamoja na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia” Dkt. Kayandabila.
Amesema kuwa kamati inatarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi, sanjari na upatikanaji wa chakula cha kutosha, na kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kutokana na shughuli za utalii pamoja na mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula.
Amesema kuwa mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sanjari na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na benki kuu katika nchi nyingi kuanza kupunguza viwango vya riba.
Amefafanua kuwa bei ya mafuta ghafi ilipungua, licha ya kuongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi Juni 2024, huku akieleza kuwa bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu, ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama uwekezaji mbadala katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi.
Amefafanua kuwa mikopo ya sekta binafsi nakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia16.4 ikilinganishwa na asilimia17.1 katika robo iliyotangulia.
“Sekta ya benki imendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha huku ikitengeneza faida na amana, rasilimali na mikopo imeendelea kuongezeka, ubora wa rasilimali za benki umeendelea kuimarika, kufuatia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu hadi asilimia 4”
Dkt. Kayandabila amesema kuwa mikopo ya sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuongezeka katika kipindi kijacho cha mwaka 2024 kutokana na kuimarika kwa hali ya uchumi wa dunia na wa ndani.
Amesema kuwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali umeendelea kuwa wa kuridhisha huku ukichagiza utekelezaji wa sera ya fedha.
Mapato ya ndani kwa Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia asilimia 95 ya lengo, huku upande wa Zanzibar, mapato yanakadiriwa kuvuka lengo kwa asilimia 0.3 kutoka na maboresho katika usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa utayari wa wananchi kulipa kodi katika mwaka 2024/25.
Dkt. Kayandabila amesema kuwa akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha kwa kuwa na zaidi ya dola za marekani bilioni 5, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa zaidi yamiezi 4.
Amesema kuwa upatikanaji wa fedha za kigeni uliimarika kiasi, mwishoni mwa mwezi Juni 2024, kutokana na ongezeko la fedha za kigeni kutoka kwenye mauzo ya tumbaku, dhahabu na shughuli za utalii.