Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson (wa kwanza kulia) akitembelea banda la Chuo hicho Kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimesema kitaendelea kufanya tafiti zenye lengo la kutatua matatizo yaliyopo katika jamii ili kuleta tija kwa Taifa katika kufanisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza Julai 3, 2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Naibu Makamu Mkuu Chuo Kikuu Cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson amesema kuwa tafiti zina mchango mkubwa katika kufika malengo ya kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
“Tafiti zetu zimelenga kuisaidia jamii kwa kutatua matatizo yaliyopo, katika maonesho haya tumekuja na mashine ambazo zinasaidia katika sekta ya samaki. Lakini wanafunzi wetu wameingia katika uwanja wa kutengeneza ‘rockets’ na kwenye maeneo ya vyakula ili kutibu maradhi kwa kutumia lishe asili,” amesema Profesa Anderson.
Profesa Anderson amesema katika maonesho ya sabasaba ya mwaka huu wameleta bidhaa mpya ambazo zimetengenezwa na wanafunzi pamoja na wanataaluma kupitia tafiti mbalimbali walizofanya.
Aidha Profesa Anderson amesema kuwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wanatarajia kufungua Kampasi mpya katika Mkoa wa Njombe itakayoanza kutoa mafunzo mwaka wa masomo 2026/2027.
Amesema kuwa kupitia mradi wa HEET Chuo kilipokea Dola za Marekani milioni 23 ambapo zinatumika kujenga miundombinu ya madarasa, maabara pamoja na kufungua kampasi mpya ili kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa jamii.
“Kampasi ya Njombe itajikita kutoa mafunzo katika eneo la misitu, madini, uvuvi na kuziboresha zaidi sekta zilizopo katika mkoa huo jambo ambalo litakuwa na tija katika kufikia maendeleo” Profesa Wineaster.
Amebainisha kuwa mafanikio yaliyopo katika chuo hicho yamechangiwa na kuwepo kwa miundombinu mizuri ya kujifunzia na kufundishia hatua inayowawezesha wanafunzi wanaofika chuoni hapo kufanya vema katika masomo yao.