NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba amesema, thamani ya Mfuko huo imepaa na kufikia trilioni 8.5, kwa hesabu ambazo hazijakaguliwa kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2024.
Ameyasema hayo Julai 3, 2024, mbele ya waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Salaam, kwenye viwanja vya Julius Nyerere, maarufu Sabasaba.
“Niwape uhakika wanachama, Mfuko uko imara na unaendelea kukua kwa kasi, miaka mitatu tu iliyopita ukuaji wa Mfuko umekuwa mkubwa mno, mwaka 2021 ulikuwa na thamani ya trilioni 4.8, tumetoka hapo hadi kufikia trilioni 8.5, ni ukuaji wa zaidi ya asilimia 77.” Amefafanua.
Bw. Mshomba ametaja sababu za mafanikio hayo kuwa ni pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mara tu baada ya kuingia madarakani alikuja na mpango wa “Kuifungua Nchi” akilenga kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza nchini
“Kichocheo kikubwa ni Mheshimiwa Rais alivyoweza kuwavuta wawekezaji, kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na waajiriwa, uchangiaji umeongezeka, vipato vya wafanyakazi vimeongezeka na haya yote yamechangia kuongeza michango na kufanya kipato cha Mfuko kutokana na uwekezaji kuongezeka pia.” Alifafanua Bw. Mshomba
Alisema sababu nyingine ni juhudi kubwa zilizowekwa na Mfuko katika kuboresha mifumo ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha utoaji wa huduma.
Aidha Bw. Mshomba amesema “Kulingana na Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unaishia Juni 2026 thamani ya Mfuko itafikia zaidi ya trilioni 11.5 na yote haya yanatokana na msukumo wa kuongeza waajiri na waajiriwa wanaochangia katika Mfuko lakini pia kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa Mfuko.” Alifafanua
Kauli mbiu ya Maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi leo Julai 3, 2024 na Rais wa Masumbiji Mhe. Filipe Nyusi akisindikizwa na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Tanzania Sehemu Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la NSSF, Julai 3, 2024.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, akimuhudumia mwanachama.