Na Sophia Kingimali.
WAKALA wa Nishati Vijijini(REA), inatarajia kutumia Sh. Bilioni 35.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa matumizi ya nishati safi yakupikia katika magereza 129 nchini katika kipindi cha miaka mitatu.
Lengo la mradi huo ni kupunguza matumizi ya nishati inayoharibu mazingira kwenye taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100.
Hayo yamebainishwa leo Julai 4,2024 na Mhandisi Mwandamizi wa REA, Deusdedit Malulu kwenye maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara yanayifanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Malulu amesema wanatarajia kushirikiana na magereza zote nchini kwa ajili ya kujenga miundombinu itakayowezesha magereza kutumia nishati safi ya kupikia.
“Tutawezesha magereza 129 yaliyopo Tanzania Bara ambapo asilimia 75.4 ya fedha za mradi huo itatoka REA na magereza wenyewe watatoa asilimia 24.6,”Amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo utagharimu sh bilioni 35 ambapo REA itatoa sh bilioni 26.5 na magereza watachangia sh bilioni 8.6 kwa miaka mitatu.
Amesema mradi huo utakaofanyika kwa awamu ambapo tayari hatua za awali zimeanza.
“Pamoja na miundombinu hiyo tutawajengea miundombinu inayotumia biogas kwa ajili ya kupikia, tutagawa mitungi ya gesi 15,920 kwa watumishi wa magereza ili waweze kutoka kwenye matumizi ya kawaida watumie gesi,”amesema.
Mhandisi Malulu aliongeza kuwa REA itaziwezesha magereza fedha kwa ajili ya kununua mitambo 61 ya kutengeneza mkaa mbadala.
Amesema magereza hutumia kuni,mkaa pamoja na nishati zingine chafuzi kwa mazingira hivyo REA itatoa majiko yanayotumia kuni kidogo au mkaa na kuni mbadala 977.
Amesema wamejipanga kutoa elimu ya matumizi ya mitambo na majiko watakayotoa katika utekelezaji wa mradi huo.