Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Dodoma.
Ni ndoto ya kila mtu kuishi maisha mazuri, akimudu mahitaji ya msingi na ya ziada. Ndoto hizo ndizo zinazowasukuma watu kufanya kazi kwa bidii maofisini, migodini, bandarini, viwandani, mashambani, baharini (uchumi wa buluu), michezoni na kwingineko ili kupata kipato cha kuwawezesha kumudu maisha yao na ya wategemezi. Ni katika hali hii ya kila mtu ya kutaka mkono uende kinywani ndiyo inayowasukuma watu kuamka alfajiri na kurudi nyumbani usiku kutoka katika mishughuliko ya kusaka fedha. Ni hali hii hii inayofanya watu kulala saa chache nje ya zile saa nane zinazoshauriwa kiafya. Kwa hakika mafanikio ya kiuchumi ni vita, ni lazima kupambana hadi tone la mwisho kuweza kufikia maisha bora.
Baadhi ya vitabu vya dini vinafundisha kwamba riziki hutolewa Mwenyezi Mungu lakini kwa utaratibu wa zama zetu lazima utafute sababu ya kuipata hiyo riziki ambayo hakuna namna nyingine isipokuwa kufanya kazi. Kwamba zama za umma wa Nabii Mussa ndio walipata bahari hiyo ya kushushiwa riziki moja kwa moja kutoka mbinguni (Mana), utaratibu ambao Mwenyezi Mungu alishaufuta.
Hebu fikiria kama utakuwa umekaa sebuleni kwako, mara unaona mikate inashuka kutoka mawinguni ikitoboa paa na kuanguka sakafuni au mezani pwaa! Mara unaona misamaki, mayai na kadhalika vikishuka. Bila shaka utatoka nduki kama wanavyosema vijana kwa sababu si utaratibu wa sasa. Lakini ili uvipate hivyo, lazima upige mzigo. Hakuna njia ya mkato.
Kimsingi, suala la mafanikio ya kiuchumi iwe kwa mtu binafsi, jamii au nchi lina kanuni zake za msingi za kuzisimamia na kuzitekeleza ili kuweza kufikia mafanikio halisi. Ni muhimu kufanya kazi kwa bidii na yale mapato yanayopatikana kutokana na kufanya kazi kwa bidii yanapaswa kuwekezwa katika nyanja mbalimbali mathalani katika kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, viwanda na kadhalika ili kuzalisha na kuongeza mapato zaidi na hatimaye kupata utajiri.
Ndugu zangu Watanzania, makala haya yana lengo la kuwakumbusha wananchi wenzangu kuwa pamoja na kiu tuliyonayo ya kupata utajiri na mafanikio makubwa ya kiuchumi ili kuishi kwenye nyumba nzuri, tule chakula bora chenye virutubisho muhimu vya kujenga afya, tuvae mavazi mazuri, watoto wetu wasome shule nzuri, tuendeshe magari mazuri, tuwe na miradi mingi ya kutuongezea kipato, siri ni kufanya kazi kwa bidii na kutumia mapato yatokanayo na kazi zetu kuwekeza na si kuamini katika imani za kishirikina kama njia ya kutufanikisha kiuchumi. Kwa nini nasema haya?
Wapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa wanaweza kupata utajiri kupitia njia za ushirikina ikiwemo kutumia majini na vinyamkera vingine. Siyo utajiri pekee, bali hata nafasi za kuchaguliwa au kuteuliwa na wakubwa wapo wanaoamini wanaweza kufika huko kwa njia za giza.
Hasa wakati huu tunaoelekea kwenye chaguzi za serikali za mitaa na baadaye uchaguzi mkuu, wenye mawazo haya ya kipumbavu wanawaza wakamwone mganga gani. Na waganga matapeli wanakula sana fedha za washirikina hawa.
Mbaya zaidi, kuna wenzetu wanaodanganywa kwamba viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) husababisha utajiri au mafanikio ya maisha ikiwemo uongozi. Huu ni ujinga wa hali ya juu kabisa.
Hebu jiulize, kama ualbino ungekuwa unasababisha utajiri si wazazi wenye watoto maalbino si wangekuwa matajiri wakubwa au mawaziri kama si marais kabisa katika nchi zao! Ni dhana potofu inayopaswa kupuuzwa na kupigwa vita na kila mwananchi mwenye upendo wa dhati dhidi ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na biandamu mwingine yeyote.
Kuamini katika viungo vya mwili kama msingi wa utajiri ni uvivu wa kufanya kazi na uvivu wa kufikiri kwa kina. Kiufupi ni danganya toto, changa la macho (udanganyifu). Wanachofanya baadhi ya matapeli kwenye matunguli yao ni kupiga ramli chonganishi kwa kuwaaminisha watu kuwa endapo watafanikiwa kupata viungo vya mwili vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi, basi wanaweza kuuaga umaskini na kuwa matajiri. Ujinga mtupu.
Ni katika muktadha huu, Mei 30, 2024, katika Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera, mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) alinyakuliwa kutoka mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana na siku 19 baadaye mwili wa mtoto huyo ulipatikana ukiwa umefungwa kwenye kiroba cha sandarusi, akiwa amefariki huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimenyofolewa.
Benjamini Mwikasyege, ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba alisema “Tumekuta mwili umekatwa baadhi ya viungo vya mwili na kutelekezwa, ila niwahakikishie Jeshi la Polisi wana wataalamu, watafanya uchunguzi wa kina, kisha tutawajua wahusika.”
Ni jambo la kusikitisha sana kuona mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu, malaika wa Mungu asiye na hatia wala dhambi yeyote akiuawa kikatili kisa tu ulemavu wake wa ngozi.
Hivi ni kwa nini binadamu tumekuwa na mioyo ya kikatili na ya kinyama kuliko hata wanyama wenyewe kwa kufanya mauaji ya raia wasio na hatia ili tu tupate utajiri? Baadhi ya watu wanaacha kujituma kufanya kazi ili wapate utajiri na badala yake wanaua wenzao, huku mwisho wao ukiwa mbaya – wanaishia jela huku wakikosa utajiri walioutarajia kupitia imani potofu za kishirikina.
Kama hiyo haitoshi, mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi, Kazungu Julius mkazi wa Katoro mkoani Geita amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana na kisha kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kuvuja damu nyingi. Mtoto huyo alivamiwa wakati akitoka kuoga ambapo mtu asiyejulikana alimkata maeneo mbalimbali ya mwili wake kama vile kichwani, sehemu za mkono na kwenye kidole cha mkono, hali iliyosababisha mtoto huyo kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani zake. Mtoto huyo amefikishwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Ni vyema ndugu zangu Watanzania tukajikita kufanya kazi kwa bidii ili tufanikiwe kimaisha. Kila mmoja atumie elimu, kipaji na kipawa alichonacho katika kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia fedha za kuweza kuendesha maisha na mipango yake aliyonayo. Hakuna uhusiano wa viungo vya mwili vya watu wenye ulemavu wa ngozi na kupata utajiri, hakuna, hakuna, narudia tena hakuna. Nina hakika hakuna anayeweza kuonesha kwamba yule katajirika kwa ajili ya kiungo cha albino.
Kwa kuwa pia hakuna kazi yenye kipato kinachoweza kutosheleza mahitaji, ni vyema pia kuwekeza katika miradi mikubwa, ya kati na midogo kadri ya uwezo alionao mtu ili kujiongezea vipato zaidi na kuepukana na tamaa ya kutaka utajiri wa haraka unaopelekea mauaji ya watu wasio na hatia. Haki ya kuishi (right to life) ndiyo haki kubwa kuliko zote, hakuna haja ya kukiuka haki hii kwa kuua wengine kwa tamaa ya mali na utajiri.
Nisisitize kuwa wale wote wanaothibitika kuhusika na mauaji haya, ni vyema hatua kali za kisheria zikachukuliwa dhidi yao ili kuwa funzo kwa wengine wenye tamaa za utajiri wa mkato na wa haraka haraka. Ndugu Watanzania wenzangu, ni wakati wa kumrudia Mungu na kuwa na hofu ya Mungu.
Hofu ya Mungu itatuongoza kuacha kabisa mauaji dhidi ya binadamu wenzetu na badala yake tutawapenda na kuwatakia kila la heri katika maisha yao. Tujue haya maisha si ya milele na hivyo kuna siku tutasimamishwa kwenye mahakama ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake ni kali na yenye kuendelea. Duniani tunapita tu. Tuchape kazi kwa bidii kwani huo ndiyo msingi wa mafanikio na utajiri na si imani za kishirikina.
Tupendane, tusifanyiane mabaya kwani Mungu aliyetuumba hapendi hayo bali anataka tupendane bila kubaguana. Tuungane kwa pamoja, kupinga mauaji haya ili kila mmoja afurahie haki ya kuishi na kufikia malengo yake aliyonayo. Tuache tamaa, kwani Tanzania bila mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, na watu wengine wote kama watoto, vikongwe inawezekana kabisa.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni : 0620 800 462.