Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayetoa huduma katika wodi za wagonjwa maalumu (VIP ward) Odilia Njau akimjulia hali raia wa Ujerumani Zsuzsanna Bona aliyepata tatizo la mshtuko wa moyo wakati anapanda mlima Kilimanjaro na kufikishwa katika taasisi hiyo kwaajili ya matibabu.
Picha na: JKCI
…………………..
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
04/07/2024 Raia wa Ujerumani aliyekuwa akifanya utalii wa kupanda mlima Kilimanjaro tarehe 24 mwezi Juni mwaka huu ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwere (JKCI) kwa kuyaokoa maisha yake baada ya kupata tatizo la mshtuko wa moyo wakati akipanda mlima huo.
Zsuzsanna Bona mwenye umri wa miaka 69 amezitoa pongezi hizo leo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam.
Alisema alijisikia vibaya wakati anapanda mlima Kilimanjaro kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania kwaajili ya kupanda mlima huo lakini kwa bahati mbaya hakuweza kufika kileleni kutokana na kupatwa na tatizo hilo.
Zsuzsanna alisema kabla ya kupanda mlima Kilimanjaro akiwa nchini Ujerumani alijiandaa na mazoezi lakini pia alifanya vipimo mbalimbali vya afya kuona kama ana tatizo linaloweza kumzuia kupanda mlima na baada ya vipimo kuonyesha hana tatizo alifika Tanzania akiwa na shauku ya kupanda mlima Kilimanjaro na kufika kileleni.
“Ilikuwa ni usiku nilipopata tatizo la mstuko wa moyo wakati napanda mlima Kilimanjaro, nilianza kuchoka ghafla na kukosa pumzi ya kutosha, mume wangu akaongea na waongoza watalii kwaajili yakunisaidia ambao walichukua hatua ya haraka kunishusha na kunikimbiza Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) ambao walinipa rufaa kufika JKCI”.
“Nawashukuru sana wataalamu wa JKCI kwani baada ya kunifanyia vipimo na kuona tatizo walinipatia matibabu ya haraka na sasa nimepona leo usiku narejea nchini Ujerumani”, alisema Zsuzsanna.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smita Bhalia alisema Zsuzsanna alifanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro na kufikia futi 4300 ambapo alipata tatizo la mstuko wa moyo kutokana na mshipa wake wa damu wa moyo upande wa kulia kuziba kwa asilimia 100.
Dkt. Smita alisema baada ya JKCI kumpokea walimfanyia vipimo na kumuingiza katika chumba cha upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab ambapo mshipa wake wa damu wa moyo upande wa kulia ulizibuliwa na sasa damu inapita vizuri.
“Kutokana na mshipa huo wa damu kuziba kwa asilimia 100 kama tusingempatia matibabu ya haraka angeweza kupoteza uhai wake, tunaishukuru Serikali yetu kwa kuwekeza katika vifaa tiba na wataalamu kwani tunauwezo wa kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya moyo”,. alisema Dkt. Smita