Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Bw. John Nchimbi.
……………………
Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya leo tarehe 3 Julai, 2024 imekutana na wawekezaji kutoka Kampuni binafsi ya BA Prerna CleanEarth kujadili uwezekano wa kuwekeza katika dampo la Nsalaga na kuzalisha mbolea inayotokana na taka ninazooza.
Mwakilishi wa Kampuni hiyo kutoka Gujarat India Bw. Parish Kalathia, amesema endapo Jiji litaridhia, kampuni hiyo itachakata taka hizo kwa kutenganisha taka ngumu na zile zinazooza na kisha kuzalisha mbolea zinatotumika mashambani.
Amesema mbolea inayotokana na taka zinazochakatwa haitakuwa na madhara yoyote kwenye ardhi na mimea itakayozalishwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji Bw. John Nchimbi amemshukuru Rais wa Mabunge Duniani, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa jitihada anazozifanya za kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza mkoani Mbeya. Jiji limepokea ombi hilo la ushirikiano na kueleza kuwa suala hilo litafikishwa ngazi za juu na endapo itaridhiwa taratibu nyingine zitafuata ikiwa ni pamoja na kusaini mkataba wa mashirikiano.
Bw. Nchimbi amesema uwekezaji kama huu umefanyika Kilimanjaro na Dar es Salaam na kuleta mafanikio.
“Uwekezaji huu mbali ya kuwa chanzo cha mapato endapo utaridhiwa pia utawanufaisha wakulima kwa kupata mbolea bora na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao mbalimbali,” amefafanua Bw. Nchimbi.