*Kata ya Buganzo wilayani Kahama kufikishiwa umeme kabla ya tarehe 5 Julai
*Mbunge wa Msalala aishukuru Serikali
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini kwa Awamu tofauti ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania Bara vitafikiwa na huduma ya umeme.
Ameeleza hayo leo Tarehe 2, Julai 2024 alipokuwa katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya umeme katika Vijiji vya Buganzo, Gura na Mwakata vilivyopo katika Jimbo la Msalala Wilaya ya Kahama.
Aidha Naibu Waziri Kapinga ameongeza kuwa hadi kufikia tarehe 5, Julai 2024 kata ya Buganzo umeme utakuwa umeshawafikia na kijiji cha Bukwangu tarehe 10 kitapatiwa umeme na kwamba Serikali inawasimamia kwa umakini Wakandarasi.
Naibu Waziri amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini kwa lengo la kuharakisha maendeleo kwa Wananchi hivyo na wao wanapaswa kusaidia kulinda miundombinu hiyo ili iwanufaishe wananchi wengi na kwa muda mrefu.
“Msiruhusu upenyo wa mtu yeyote kuhujumu miundombinu, tuhakikishe tunailinda kwani Serikali imewekeza fedha nyingi hivyo tuipe thamani inayostahili.” Amesema Naibu Waziri Kapinga
Pia Mhe. Kapinga amesema Serikali ya Awamu wa Sita ni ya maendeleo hivyo wananchi wanapaswa kutumia huduma ya upatikanaji wa umeme vijijini kujiinua kiuchumi kwa kuutimia katika shughulli za biashara.
“Tupo makini sana na utekelezaji wa miradi ya umeme tunaitaji nyinyi wananchi muweze kubadilisha mfumo wenu wa maisha ili kila mtu aongeze thamani katika kile anachokifanya kwa ajili ya maendeleo ya maisha yenu ndio maana tupo hapa kwaajili ya kuhakikisha tunawafikishia umeme wa uhakika.” Amesema Kapinga
Pia, Naibu Waziri Kapinga amewataka wakandarasi wanaojenga miradi ya REA kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Amesisitiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga kuitumia vizuri fedha iliyotengwa ya Shillingi Milioni 78 kuvipatia vijiji umeme wa uhakika haswa katika maeneo ya Taasisi ikiwemo za Dini.
” Nitafuatilia kuhakikisha Umeme unazifikia Taasisi ikiwemo za Dini ili wananchi waweze kufanya Ibada kwa furaha huku wakimwabudu Mwenyezi Mungu.” Amesisitiza Kapinga
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Iddi Kassim, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kufikisha umeme katika Vijiji hivyo na kusema kuwa umeme huo utaongeza fursa kwa Wananchi katika utekelezaji wa shughuli Mbalimbali za Maendeleo.