BOHARI ya Dawa (MSD), imedhamiria kuleta mageuzi makubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maghala katika mikoa mbalimbali ili kufanikisha malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta ya afya.
Hayo yamebainishwa na
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai wakati akizungumza na wahariri mkoani Dodoma mara baada ya kukamilisha ziara ya kujionea ujenzi wa maghala na uendeshwaji wa kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono kilichopo Makambako mkoani Njombe.
Amesema kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.
Amesema kuwa katika kuimarisha utendaji wake na uwekezaji wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhiwa dawa na vifaa tiba itaendelea na ujenzi wa maghala katika kanda ili kurahisisha utoaji huduma kwa wateja.
Mavere amesema kuwa Bohari ya Dawa inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 8,224 kutoka vituo 7,662 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la vituo 562 nchini kupitia Kanda zake 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.
Pamoja na hali hiyo amesema kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.
Ameyataja mafanikio hayo kuwa ni kuongezeka kwa utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya hasa kwa Dawa,Vifaa,Vifaa Tiba na Vitendanishi.
Amesema Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya yanatimizwa kwa mujibu wa maombi yao. Kutokana na kuimarika kwa utendaji, utimizaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma za afya umeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2022/23 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2023/24 na hivyo bidhaa nyingi kuweza kupatikana kupitia MSD.
“Bohari ya Dawa (MSD) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa Na.13 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021 ikiwa na majukumu manne ambayo ni Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za umma na binafsi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.
“Sambamba na hilo, MSD imeendelea kufanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi nchini kama mashine za kusafisha damu (Dialysis Machine), MRI, CT- Scan, Ultrasound, Digital X-Ray pamoja na vitendanishi vyake. Uwepo wa vifaa hivi unawezesha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi,” amesema Tukai
Kutokana na hali hiyo Mkurugezi huyo wa MSD amesema kuwa mafanikio mengine ni kupatikana kwa mtaji wa uendeshaji kiasi cha Shilingi bilioni 100 kwa mwaka wa Fedha 2023/24, Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 100 kama mtaji wa kuwezesha MSD kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi.
Amesema fedha hizo zimesaidia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati na kuweza kutengeneza mikakati itakayofanya taasisi iweze kununua kwa tija na kuimarisha mahusiano na wazabuni mbalimbali.
“Kuimarika kwa makusanyo ya fedha kutoka vituo vya kutolea huduma za afya ikiwamo maboresho yanayoendelea yamewezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na imani na utendaji wa MSD ambapo makusanyo ya fedha yatokayo kwenye vyanzo mbalimbali vya vituo vya kutolea huduma za afya na kuletwa MSD yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 40.3 mwaka 2022/23 na kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 118.9 kwa mwaka 2023/24.
“Kuongezeka kwa Mapato ya MSD kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali, Mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 359.6. kwa mwaka 2022/23, hadi kufikia zaidi ya kiasi cha Shilingi bilioni 510.07 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 150.43 ambayo ni sawa na asilimia 42,” amesema.