Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Ilonda akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3, 2024, Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linatarajiwa kufanya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya mazoezi ya kivita katika maeneo mbalimbali nchini kabla ya siku ya kilele.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3, 2024 jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la JWTZ Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, amesema kuwa maadhimisho hayo yataenda pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii kama vile utoaji wa matibabu ya afya kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano na jeshi tangu kuanzishwa kwake.
Luteni Kanali Ilonda amesema kuwa hospitali za Kanda za Kijeshi kutoka Mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mwanza, Mbeya, Tabora, Zanzibar, zitatoa matibabu bure kwa wananchi ikiwemo magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI pamoja na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Shinikizo la Juu la Damu, Saratani ya Matiti, Tezi dume, Sukari, Maabara na Damu salama na magonjwa ya dhalura.
“Kutakua na mazoezi mbalimbali ya kivita yatakayofanyika katika Mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Tanga na Morogoro, hivyo amewaomba wananchi wasiwe na hofu wakati watakapoona zana za kivita ikiwemo vifaru na ndege zikipita katika makazi yao” amesema Luteni Kanali Ilonda.
Luteni Kanali Ilonda amewatoa hofu wananchi wanapoona zana za kivita zinapita kwenye maeneo ya makazi yao wasiwe na wasiwasi kwani zana hizo zinatumika katika zoezi ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi lao ambapo mwaka huu wamepanga maadhimisho haya yawe ya aina yake tofauti na maiaka mingine.
Luteni Kanali Ilonda amesema katika maadhimisho hayo Jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ) litashirikiana na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa china kufanya zoezi ya pamoja kuanzia Julai 29 hadi Agost 11,2024 katika maeneo ya mkoa wa Dar es salaam na Pwani.
Amesema kuwa vikosi vitakavyohusika katika zoezi hilo ni pamoja na Kamandi ya Maji, Kamandi Nchi kavu, Kamandi ya Anga ambapo watatumia zana ikiwemo meli na ndege za kivita.
”JWTZ na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China litakua ni kuwakumbuka waasisi wa majeshi haya akiweo Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa China wa awamu hiyo, pia kumbukumbu ya miaka 60 ya udugu na uhusiano wa mataifa haya mawili” amesema Luteni Kanali Ilonda.
Amesema zoezi hayo yatafanyika baharini na nchi kavu katika eneo la wazi ili wananchi wapate fursa yakujionea kupitia vyombo vya habari kwa wale ambao hawapo maeneo ya baharini.
Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake Septemba Mosi mwaka huu kwa kufanyika kwa gwaride maalumu pamoja na kuonyesha silaha za kivita tangu JWTZ ilivyoanza na ilipo hivi sasa katika kuimarisha ulinzi wa Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shughuli nyingine zitakazofanyika katika maadhisho hayo ni pamoja na mashindano ya utamaduni kwa ajili ya kukuza utamaduni wa mtanzania, mashindano ya Mkuu wa Majeshi, Michezo mbalimbali pamoja na Gwaride.