Na Georgina Misama, CBE, Dar es Salaam
Serikali imesema inatambua mchango unaotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara Tanzania (CBE) katika kuchochea maendeleo ya Sekta ya Biashara na ukuaji wa uchumi nchini hususan kwa kutoa mafunzo na kufanya tafiti zenye kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Akiongea mapema leo Julai 03, 2024 katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za miaka sitini (60) ya CBE zilizofanyika katika Kampasi kuu Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara Dkt. Hashil T. Abdallah alisema wahitimu wengi wa CBE wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi nchini.
“Mchango wa CBE Tanzania ni mkubwa, elimu inayotolewa hapa imesaidia katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu wahitimu wanaotoka hapa wamekuwa wakiajiriwa na kuchangia ukuaji wa viwanda na biashara ambapo ni sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” alisema Dkt. Abdallah.
Aidha, Dkt. Abdallah alimuahidi Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Prof. Wineaster Anderson pamoja na uongozi wa Chuo kuwa wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha Chuo kinatimiza malengo yake kwa ubora na kwa wakati.
Kwa upande wake Prof. Anderson aliishukuru Serikali kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho kwa kipindi cha miaka mitatu na kwamba ndani ya muda huo Chuo kimeendelea vizuri na kwamba kinaendeshwa kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa.
“Mhe. Mgeni Rasmi, kwa niaba ya Bodi ya CBE tunakushukuru wewe na Wizara yako kwa kuiamini Bodi iliyokuwepo kwa miaka mitatu, hivi sasa Chuo kinaendelea vizuri, Wanafunzi na Wafanyakazi wameendelea kutunza nidhamu ya kazi na taaluma na viongozi wameendelea kusimamia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya nchi na taasisi, aidha Bodi imeendelea vizuri pia,” alisema Prof. Anderson.