Na Sophia Kingimali.
Wanafunzi kutoka mikoa mitano Bara na Visiwani wanatarajia kutembelea Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) ili kupata ujuzi zaidi kwa vitendo.
Hayo yamebainishwa leo Julai,1 2024 na Afisa Utamaduni wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Chance Ezekiel wakati Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula alipotembelea banda lao lilopo kwenye maonesho ya 48 maarufu kama sabasaba.
Amesema wanafunzi wanatarajia kufika kwenye makumbusho hayo Julai, 5 2024 ambapo wanafunzi kutoka Zanzibar hadi sasa wanafunzi 22 wamethibitisha kuwepo na bara wanafunzi 12 ambapo bado wanaendelea kujisajili hivyo, wataendelea kuongezeka kadili ya siku zinavyosogea.
“Wanafunzi watakiwa kujifunza vitu mbalimbali kwa vitendo kwasababu shule wanasoma kwa nadharia wanatakiwa kutembelea Makumbusho ya Taifa mbalimbali ili waone kwa uhalisia na kujifunza, “amesema Ezekiel.
Ameongeza kuwa wana Urithi usio shikika wa uchanjaji Chale na ndonya wa kabila la makonde umehifadhiwa kidigitali na kutoa nafasi kwa mtazamaji kupiga picha kupitia mitandao ya kijamii na kufurahia na marafik zao kwa teknolojia ya “Agumented Realty” (AR).
Ameeleza kuwa wanafungua fursa za uwekezaji na biashara kwa watanzania kwenye maeneo ya mali kale na makumbusho ikiwemo biashara ya vyakula na huduma mbalimbali kwa watalii pamoja ujasiriamali wa bidhaa za kiutamaduni na asili ya Mtanzania.
Aidha amesema utalii wa matamasha ya Utamaduni umeendelea kuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.