Na Sophia Kingimali.
Katibu Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii Dk, Hassan Abasi amesema serikali imejidhatiti kuja na uwekezaji katika utalii wa ikolojia kupitia misitu kwa sababu ya uwepo wa madhari nzuri na yenye kuvutia wageni kuja nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo julai 2,2024 na Katibu Mkuu huyo wakati alipotembelea banda la wizara ya Maliasili na utalii katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam (DITF).
Amesema uwekezaji wa utalii wa ikolojia utahusisha na ujenzi maeneo ya kupumzikia wageni pindi wanapotembelea vivutio hivyo katika maeneo ya uhifadhi.
Aidha ameongeza kuwa awali misitu ilikuw kwa ajili ya ukataji wa mbao lakini sasa imekuwa kivutio kikubwa cha utalii hivyo watu wanaweza kutembelea na kujifunza lakini pia kufurahia madhari nzuri zilizopo misituni.
“ Pia nimepita katika mabanda yetu na nimeona watu wakivutiwa na uwekezaji mwingine wa asali na nyuki kwani wanataka namna ya kuweakeza katika jambo hilo, suala hilo tunalichukua na tutaangalia namna ya kuwasaidia kupitia mfuko wa nyuki na asali,” amesema.
Amesema tafiti zilizofanywa duniani mwaka huu Tanzania imeongoza Afrika kuwa na wageni wengi wa utalii kutoka nafasi ya pili ilishika mwaka jana.
“ Bado tuna fursa nyingi za uwekezaji , takwimu zinaonyesha mwaka jana julai ya watalii kutoka nje milioni 1.8 walitembelea vivutio vyetu na watalii wa ndani ni milioni 1.9 , jumla ni milioni 3.7 hivyo tunaimani dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassani ya kuwa na watalii milioni tano tutaitimiza Desemba, mwaka huu,” amesema.
Sambamba na hayo katika kuendeleza zao la asali Katibu mkuu amesema wamekuwa wakitoa ruzuku kwa wakulima wa zao hilo.
Pia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS ) Kanda ya Mashariki imetoa rai kwa wananchi kujitokeza kwenye banda lao ili waweze kujifunza na kufaidika na ofa zinazotolewa kwa watakaohitaji kutembela hifadhi za misitu zilizopo nchini