Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga amesema ni muhimu kutumia majukwaa mbalimbali katika kusambaza ujumbe kwa jamii kuhusu teknolojia za uelimishaji kuhusu Afya ikiwemo “Tunza Afya Chat”kwa njia ya Whatsaap.
Dkt. Haonga amebainisha hayo leo Juni 29, 2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma,Idara ya Afya ya Uzazi,Mama na Mtoto na kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Development Media International(DMI) katika kikao cha kupitia Maudhui ya uelimishaji kuhusu Masuala mbalimbali ya Afya ikiwemo malezi na makuzi ya mtoto .
“Tunayemtafuta atumie Chatbot ni mwananchi hivyo kuna makundi na majukwaa mbalimbali ikiwemo ya viongozi, wanataaluma,vikundi mbalimbali ,makundi ya whatsaap ya masuala ya siasa, watu mliosoma pamoja,mnajua na walimu nao wana network namna ya kuwasiliana, mfano ukimpa mratibu wa elimu ya afya wa wilaya au mratibu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto lazima ujumbe ujumbe unafika hadi ngazi za chini kabisa”amesema.
Aidha, Dkt. Haonga amesema kwenye eneo la Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii(CHW)watahakikisha wanajengewa uwezo zaidi kuzijua teknolojia mbalimbali za uelimishaji ikiwemo mfumo wa Tunza Afya Chat kupitia Whatsaap ili kufikisha ujumbe kwa jamii.
Halikadhalika, Dkt. Tumaini ametumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la DMI kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utengenezaji wa Maudhui mbalimbali ya uelimishaji.