…………….
Iringa
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila amewataka wakandarasi wanaojenga barabara ya Mtili -Ifwagi na barabara ya Wenda-Mgama kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kusaidia wananchi kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa urahisi.
Mhandisi Mativila ameyasema hayo baada ya kukagua ujenzi wa barabara hizo ambazo zinajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 52 chini ya Mradi wa RISE.
Barabara hizo zinajengwa na Mradi wa ‘RISE’ kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ukiwa na lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu,mbogamboga, chai na mazao mengine toka mashambani kufika sokoni kwa wakati.
Mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Tanga, Geita na Lindi kwa ujenzi wa barabara Km. 500 na kuondoa vikwazo pamoja na kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara kwa kutumia wananchi wanaoishi kandokando ya barabara za wilaya nchini.