Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania (TSPA) kimesema mabadiliko ya Sheria ya Sukari ya mwaka 2020 imesaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa Sukari nchini kwa asilimia 93 kulingana na mahitaji ya Taifa ya hivi sasa tani 490,000 kwa mwaka.
Akizungumza na viongozi wa Chama wa TSPA katika Mkutano na waandishi wa habari kuhusu hali halisi ya uzalishaji wa sukari nchini Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kampuni ya Kilombero Sugar Ltd Balozi Ami Mpungwe alisema kuwa wazalishaji wa sukari kwa sasa hawahitaji biashara ya uagizaji sukari kwa kuwa wao wanazalisha, hivyo endapo serikali inaitumia NFRA kuagiza sukari nje ifanye hivyo bila kuweka mipango ya ujanjaujanja.
Amesema TSPA imetoa baraka kwa serikali kuruhusu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuagiza sukari nje ya nchi, huku wakieleza mikakati yao ya kumaliza nakisi ya bidhaa hiyo.
“Tumeumizwa sana na kauli mbalimbali potofu kuhusu sekta na kampuni za sukari nchini. Baadhi ya kauli hizi ziimelenga kuchafua na kudhoofisha kampuni za sukari mbele za umma. Tulikaa kimya kwa muda mrefu lakini leo tunasema tupo na serikali na watanzania katika hili,” alisema Balozi Mpungwe.
Alisema tangu nakisi ya sukari ilipotokea Desemba, mwaka jana kutokana na tatizo la mvua za El Nino, kampuni hizo zimekuwa mstari wa mbele kupunguza ukali wa nakisi hiyo ikiwemo kuagiza tani 50,000 kutoka nje baada ya kupatiwa vibali na serikali.
“Si kweli kwamba kampuni hizi hazikuwajibika kwamba tulipewa vibali halafu hatukuagiza sukari…kwa miaka mingi kumekuwa na uongo kwenye tasnia hii ambayo inahitaji kulindwa. Ukweli ni kwamba tunashindana na wazalishaji wakubwa wenye bei ndogo,” alieleza.
Alitolea mfano kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha tani 500,000 za sukari wakati Brazil inazalisha tani milioni 32 hali ambayo kiuchumi haiwezi kuwa sawa.
Alisema ndio maana tangu sakata hilo lilipoibuka wazalishaji hao walijaribu kuwasiliana na Kamati za Bunge za Viwanda na Biashara na ya Bajeti lakini hawakufanikiwa.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo Hussein Sufian alielezea mikakati ya wazalishaji hao kumaliza nakisi ya sukari nchini kuwa kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji mkubwa wa mitaji ya miradi wanatarajia ifikapo mwishoni mwa msimu huu wa 2024/25 kwa uzalishaji unaoendelea hivi sasa unaotarajiwa kufikia tani 528,000 na tani 663,000 kwa mwaka 2025/26.
Alisema hatua inatokana na hatua hatua madhubuti zilizochukuliwa na serikali kuvilinda viwanda na wakulima wa miwa wa ndani ambapo sasa uzalishaji wa sukari umepunguza nakisi ya sukari (Gap sugar) kutoka tani 144,000 mwaka 2017, hadi tani 30,00 tu mwaka 2023.
“Kwa ujumla, uwekezaji huu mkubwa wa viwanda vyetu umekuwa na malengo ya kimkakati ya muda mrefu ya kukidhi mahitaji ya sasa na ya zaidi ya miaka 50 ijayo,” alisema.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni mipango ya upanuzi wa viwanda na mashamba ya miwa ambapo Kilombero itaongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 127,000 hadi tani 271,000 kwa mwaka kuanzia mwezi huu
Alisema kiwanda hicho kitaongeza uzalishaji wa miwa kutoka tani 600,000 hadi tani 1,700,000 kwa mwaka, hivyo kuongeza mapato yao mara tatu. Aidha, idadi ya wakati kiwanda cha sukari cha Kagera kitaongeza uzalishaji kutoka tani 131 ,000 kwa sasa hadi tani 230,000 katika misimu mitatu ijayo.
Uzalishaji wa miwa ya wakulima utaongezeka kutoka tani 150,000 hadi tani 300,000 ifikapo mwaka 2028/29.
Kiwanda cha Mtibwa, alisema kitaongeza uzalishaji na kufikia tani 130,000 kwa mwaka ifikapo 2027 kutoka tani 64,000 kwa sasa wakati TPC kitaongeza uzalishaji kutoka tani 116,000 hadi tani 120,000 ifikap 2026/27.
Kwa upande wa kiwanda cha Bagamoyo alisema awamu ya kwanza ya uwekezaji ulizalishaji ulianza mwaka 2022 na awamu ya pili ya mradi imekwishaanza hivyo kitaongezza uzalishaji kutoka tani 30,000 za sasa hadi tani 60,000 katika miaka miwili ijayo
Alisema viwanda hivyo ni muhimu kwa kuwa vimetoa ajira kwa wafanyakazi zaidi ya 25,000 za moja kwa moja na zaidi ya 100,000 zisizo za moja kwa moja na hulipa Sh bilioni 250 kwa mwaka kwa serikali na taasisi za umma.
Aidha, alisema viwanda hivyo vinapozalisha sukari huokoa zaidi ya dola za Marekani milioni 300 kila mwaka zinazotumika kuagiza sukari nje ya nchi huku kukiwa na uwekezaji wa zaidi ya Sh trilioni 3.5 katika sekta hicho kilichowekezwa kuanzia mwaka 2015 hadi 2024.