Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Katika kutekeleza Kampeni ya Mtu ni Afya,wito umetolewa kwa jamii kuendelea kutumia namba 199 bure kwa kupiga na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya Afya ikiwemo Elimu ya Afya ya Uzazi.
Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Msimamizi wa Kituo cha Kutoa Elimu na kujibu hoja za Wananchi kuhusu masuala ya Afya cha Wizara ya Afya(Afya Call Center 199), Beatrice Titho wakati akizungumza katika Mafunzo kwa Watumishi wa Huduma ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto yanayohusu kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia Mfumo wa Taarifa wa Kituo cha Taarifa (Afya Call Center) jinsi ya kupokea maswali na hoja zinazowasilishwa na wananchi katika eneo la Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto.
“Lengo la mafunzo haya ni kujengeana uwezo namna ya kutumia mfumo wa taarifa wa Kituo cha Wizara ya Afya (Afya Call Center) kwa ajili ya kujibu hoja zinazowasilishwa na wananchi kupitia namba 199 na katika kutekeleza kampeni ya Mtu ni Afya tunaendelea kuipatia jamii elimu kuhusu masuala mbali mbali ya Afya kupitia namba 199 bila malipo”amesema.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Huduma ya Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Zuhura Mbuguni amesema mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwao namna ya kujibu hoja za wananchi wanaopiga simu bure kupitia namba 199.
“Mafunzo haya yanatija sana niwashukuru wenzetu wa UNESCO kwa kuendelea kuwezesha hivyo kupitia mafunzo haya na tuwashukuru wenzetu wa Elimu ya Afya kwa Umma sasa tutaweza kujibu hoja za wananchi katika eneo la afya ya uzazi kwa usahihi na kwa wakati”amesema.
Kwa upande wake,Mratibu wa Elimu kwa Afya na Ustawi kutoka UNESCO Mathias Faustine Luhanya amesema katika kufikia matokeo chanya ya elimu,ni lazima Watoto na vijana hususan wanafunzi na wanachuo wanakuwa na afya njema hasa katika uelewa kuhusu afya ya uzazi.
“Ili kufikia matokeo chanya ya elimu ni lazima , Watoto na vijana wawe na afya njema ,kwa kuzingatia hilo, UNESCO ikifanya kazi na Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa afya za watoto na vijana zinakuwa bora ili kuwawezesha kusoma na kufanya uelewa na stadi na mahali sahihi pa kuuliza na kupata taarifa za afya kutoka chanzo sahihi”amesema.