Na. Zillipa Joseph, Katavi
Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko ameitaka jamii kuchukua tahadhari juu ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.
Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi alisema upo umuhimu mkubwa wa kufahamu hali yako kiafya ikoje na kushauri kinamama wajawazito kuhudhuria kliniki mapema ili kupata dawa za kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa mtoto aliye tumboni endapo mama atabainika ameambukizwa virusi hivyo.
“Pia nitumie fursa hii kuwataka kinababa kutowaacha wenza wao pale wanapotakiwa kupima kliniki ili waweze kufarijiana pale mmoja wao au wote wanapogundulika wameambukizwa” alisema mkuu huyo wa mkoa wa Katavi.
Alisisitiza jamii kufahamu umuhimu wa kutambua afya zao na kuanza matibabu mapema.
Mratibu wa UKIMWI mkoa wa Katavi Dk. Solomon Tyasso alisema wakinamama wajawazito wenye kuishi na virusi vya ukimwi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawakinga watoto wao wasipate maambukizi ya UKIMWI.
“Hii yote inatokana na elimu wanayopata pindi wanapofuata dawa zao” alisema Dk. Tyasso.
Alifafanua kuwa mkoa umeendelea kuratibu mpango wa matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambapo kwa mwaka 2023 jumla ya wagonjwa 10,380 watu wazima 9,754 na watoto 616 wanaendelea na matumizi ya dawa.
Aidha, katika huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha, mkoa umeongeza vituo vya kutolea huduma ya afya ambapo mwaka 2012 mkoa ulikuwa na jumla ya vituo 49 kati ya 72 vyenye wataalamu waliofundishwa kutoa huduma kwa watu wenye VVU.
Hivi sasa kuna vituo 103 kati ya 143 vya kutoa huduma za Afya katika mkoa vyenye kutoa huduma kwa wenye virusi vya ukimwi.
Hali kadhalika hali ya maambukizi ya UKIMWI kwa mkoa wa Katavi yamepungua kutoka asilimia 5.9 mwaka 2012 mpaka asilimia 4.1 ya wakazi wa mkoa huo ambao ni milioni 1.1 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022.
Baadhi ya kinamama wajawazito wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao walikiri kupokea dawa za kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Huwa nahudhuria darasa la watu wa VVU na nilipopata ujauzito niliwaeleza na walinibadilishia makopo ya dawa” alisema mama mmoja jina linahifadhiwa.
“Kwa kweli wanatupa huduma nzuri kwanza tukija huku hospitali hawatunyanyapai kwahiyo tunahisi vizuri tu” alisema mama mwingine.
“Mimi nilipata watoto mapacha na walikuwa salama. Hakuna siku niliacha kumeza kidonge” aliongeza mwingine ambaye sasa watoto wake wana miaka miwili.
Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la Lake Rukwa Development Organization (LARDEO) Filbert Chundu amesema shirika hilo limekuwa likisaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hata wale ambao wazazi wao walipoteza maisha kwa UKIMWI.
Chundu ameeleza kuwa huwa wanafanya zoezi la kugawa lishe kwa watoto wa chini ya miaka nane wanaoishi katika mazingira magumu.
Amefafanua kuwa kwa msimu uliopita wamefikia watoto 62 wa Manispaa ya Mpanda kati yao watoto 8 wazazi wao walifariki kwa UKIMWI.
Alieleza kuwa Programu ya Taifa Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (PJT-MMMAM) inamtaka mtoto wa kitanzania kupata haki zake zote ikiwemo ya kuwa na afya bora lengo likiwa ni kuhakikisha mtoto huyu anakua kikamilifu.
Kwa mujibu wa sura ya tatu ya sera ya Taifa ya kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2001 iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu malengo makuu ya sera hiyo ni kuweka mfumo wa uongozi na uratibu wa sekta mbalimbali katika kukabiliana na VVU/UKIMWI.
Sera hii inawajibisha kila sekta kuandaa mipango inayofaa kuzuia kuenea kwa VVU na magonjwa mengine ya zinaa na kupunguza athari kwa jamii.
Pia sera hii inajumuisha taasisi za kibinafsi, kidini na NGO’s katika kukabiliana na VVU/UKIMWI.
Kwa mujibu wa sura ya tatu ya sera ya Taifa ya kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2001 iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu malengo makuu ya sera hiyo ni kuweka mfumo wa uongozi na uratibu wa sekta mbalimbali katika kukabiliana na VVU/UKIMWI.
Sera hii inawajibisha kila sekta kuandaa mipango inayofaa kuzuia kuenea kwa VVU na magonjwa mengine ya zinaa na kupunguza athari kwa jamii.
Pia sera hii inajumuisha taasisi za kibinafsi, kidini na NGO’s katika kukabiliana na VVU/UKIMWI.