Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda akizungumza katika kambi hiyo mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo,Dkt. Peter Kisenge akizungumza katika kambi ya madaktari bingwa mkoani Arusha
……..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Jumla ya wagonjwa 29,000 wamechunguzwa magonjwa mbalimbali katika kambi ya madaktari bingwa iliyowekwa katika viwanja vya Sheik Amri Abed mkoani Arusha.
Ambapo wagonjwa waliochunguzwa kwa upande wa magonjwa ya moyo ni 1,500 huku kati ya hao wagonjwa 183 wanapelekwa katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo gharama zote za matibabu hayo zinalipwa na Rais Samia Suluhu.
Akizungumza katika kambi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo,Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa ,zoezi limeenda vizuri ambapo wananchi wamepata fursa ya kuhudumiwa magonjwa na madaktari bingwa waliobobea katika maswala mbalimbali.
Dkt. Kisenge amesema kuwa,jumla ya watoto 150 wamepimwa ugonjwa wa moyo ambapo katika hao watoto 53 wanatakiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa kutokana na valve zao kupata matatizo .
“Watoto hao wote matibabu yao yatagharamiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo operesheni kwa mtoto mmoja inagharimu kiasi cha shs,12 milioni na hivyo wananchi mnapaswa kuona ni jambo la kishujaa sana lililofanywa na Rais Samia kwani kwa kawaida mwananchi wa kawaida ni ngumu sana kumudu hizo gharama.”amesema Dk Kisenge.
Aidha amesema kuwa, muda wa matibabu hayo umeongezwa hadi kesho kwa ajili ya kumaliza wagonjwa ambapo wanaendelea kupata huduma katika kambi hiyo ili waweze kupata huduma wanayostaili.
“Takwimu zinaonyesha duniani kote kuwa asilimia kubwa ya watu wanaopoteza maisha wanatokana na magonjwa ya moyo hivyo elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa ajili ya wananchi kufuata taratibu mbalimbali ikiwemo kufanya mazoezi mara kwa mara sambamba na kupunguza vyakula vya wanga na kuzingatia lishe bora.”amesema .
Hata hivyo Dk.amesema kuwa ,Taasisi hiyo ina mpango wa mkakati wa kufungua kitengo cha Moyo mkoani Arusha mwezi wa tisa kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa Arusha na kuondokana na gharama ya kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Paul Makonda amesema kuwa, anashukuru kwa namna ambavyo huduma hiyo inavyotolewa na madaktari bingwa na mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa sana .
“Haya yote yanayofanyika hapa ni upendo wa Rais Samia kwa wananchi wake kwa kupunguza gharama ya kufuata huduma hiyo jijini Dar.es Salaam kwani kwa kufanya hivyo ni faraja kubwa sana kitendo cha kuona matatizo ya watu sio jambo la kawaida ,tumuombee sana Rais Samia kwani anapambana na changamoto za wananchi kwa kiwango kikubwa sana .”amesema Makonda.
Nao wananchi waliohudumiwa katika banda hilo la JKCI ,Tabu Juma amemshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo amewezesha uwepo wa kambi hiyo ambapo mume wake ameweza kupimwa na kugundulika mishipa yake imepanuka na kuweza kupatiwa dawa kwani anaishi maisha ya shida na ingekuwa ngumu sana kupata matibabu kutokana na gharama hiyo.