Na. Zillipa Joseph, Katavi
Mkoa wa Katavi umeendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi yaani MMAM, ambapo hadi kufikia mwezi mei mwaka 2024 umeweza kujenga jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 143 ikiwemo hospitali ya Rufaa ya mkoa, kutoka zahanati 69 mwaka 2012.
Hali hiyo imewezesha kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na kuhakikisha afya ya mama inaimarika hasa wakati wa ujauzito.
Sista Elida Machungwa ni Mratibu wa Afya ya mama na Mtoto mkoa wa Katavi amesema hadi kufikia mwaka 2023 vifo vya watoto wachanga vimepungua hadi kufikia vifo vinne kwa watoto 100,000 wanaozaliwa hai.
Sista Machungwa amefafanua kuwa hali hiyo inatokona na maboresho yaliyofanyika kwa wahudumu wa afya kwa kuongezewa ujuzi na pia wananchi kuwahi kumfikisha hospitali mama mwenye uchungu.
“Vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano vimepungua kutoka watoto 83 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2012 hadi kufikia vifo vinne kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2023” alisema.
Kufikia mwaka 2024 mkoa wa Katavi umekuwa na vituo vya kutolea huduma ya afya 143 zikiwemo hospitali za wilaya tano, vituo vya afya 28, zahanati 106 na hospitali ya rufaa moja.
Aidha huduma ya usafirishaji wa mama mjamzito kumwahisha hospitali kwa ajili ya kujifungua (M-MAMA) nayo pia imeongeza mchango wa akinamama kujifungua salama na hivyo kuokoa watoto wachanga.
Bi. Lucia Mang’ulizi ni mkazi wa Shanwe katika Manispaa ya Mpanda. Anasimulia hadithi yake ya ujauzito na kueleza kuwa alikuwa akihudhuria kliniki mara kwa mara.
Lucia anaeleza kuwa ulipofika wakati wa kujifungua alifikishwa hopsitalini na njia yake ya uzazi iliposhindikana kufunguka alilazimika kufanyiwa upasuaji na kupata mtoto wa kike ambaye sasa mtoto huyo ana miezi minne.
Kwa upande wake bwana Khalfan Lumbwe mkazi wa Kasangantongwe katika halmasahuri ya Tanganyika alisimulia kuwa kipindi cha miaka ya nyuma mkewe alipoteza ujauzito mara tatu.
Anakiri kuwa huduma za hospitali zimemwezesha sasa kuwa na watoto wawili ambapo anaeleza kuwa mkewe alifanikiwa kupata mapacha mwaka uliopita.
Dokta Jonathan Budenu ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Katavi ametaja sababu kuu iliyokuwa inapelekea vifo vya watoto wachanga kuwa ni pamoja na kuwa mbali na vituo vya kutolea huduma za afya.
“Sababu nyingine ni mama kuchelewa kufika hospitali anapokuwa na uchungu na suala la kujifungulia majumbani wakunga wa jadi kukosa utaalamu wa kutosha pale mama anapotokwa na damu nyingi” alisema Dk. Budenu.
Katibu Tawala mkoa wa Katavi bwana Albert Msovela ameendelea kuwataka wakazi wa mkoa huo kuzingatia kanuni za afya na kuhakikisha kinamama wajawazito wanahudhuria kliniki.
“Kliniki zinasaidia kutoa elimu mbalimbali kuanzia namna ya kula vyakula vyenye lishe bora mpaka kuwaandaa kinamama kwa ajili ya kuwahi vituo vya afya pale uchungu unapoanza” alisema.
Wakati huo huo Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto inaeleza kuwa wanawake wenye msongo wa mawazo kipindi cha ujauzito wana uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto wenye uzito mdogo au kuzaa watoto njiti.
Hali hiyo inatokana na msongo wa mawazo wa mama na kupelekea ukuaji wa mtoto kuchelewa ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto na kuchelewa kuongea hasa wa umri wa miaka 0-8.
Askofu Ephraim Ntikabuze ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya LARDEO yenye dhamana ya kuchagiza malezi na makuzi ya awali ya mtoto kwa mkoa wa Katavi ametoa rai kwa jamii kutambua kuwa malezi ya mtoto yanaanza na jamii yenyewe.
Askofu Ntikabuze ameitaka jamii inapokuwa karibu na mama mjamzito kuhakikisha inampa faraja ya kutosha.
“Pia mama mjamzito hapaswi kuachiwa majukumu yote ya nyumbani anapozidiwa na kazi inaathiri ujauzito wake” alisema askofu Ntikabuze.
Kwa mujibu wa sera ya afya iliyotolewa na Wizara ya Afya mwaka 2007 kipengele namba 19.5 tamko la sera linaweka wazi kwamba Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha afya ya uzazi ya wanawake na wanaume, watu wenye ulemavu, vijana na wazee.
Pia serikali itaandaa miongozo, mikakati na kuratibu shughuli zinazolenga afya ya uzazi ya makundi mbalimbali pamoja na kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango unatekelezwa.
Aidha serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha utoaji wa huduma bora za uzazi katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazowavutia wanawake, wanaume na vijana.
Hivyo basi jitihada za serikali za kuboresha huduma za afya zinaonekana wazi kwa kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma hiyo ambapo katika kila kituo cha afya kumekuwa na msisitizo wa kuwepo kwa jengo la mama na mtoto.