Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba NHC, Bw. Hamad Abdallah amesema shirika hilo linaendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati na chini kupitia mradi wa huo Samia Scheme unaojengwa eneo la Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es Salaam ambapo utekelezaji wake unaendelea.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam mara baada ya Mwenyekiti wa KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava kutembelea miradi huo na mingine miwili ambayo ni Kawe711 uliopo Kawe na Morocco Square yote ikiwa jijini Dar es Salaam.
Amesema mradi huu wa Samia Scheme ni mradi wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anayofanya Rais Samia ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora nchini.
Amesema asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa katika mkoa wa Dar es Salaam ,asilimia 20 mkoa wa Dodoma na 30 mikoa mingine.
“Mradi huu wa Samia Scheme utakuwa na nyumba 5000 ambapo utatekelezwa kwa awamu na utagharimu kiasi cha shilingi .bilioni 466 sawa na dola za kimarekani milioni 200, katika kuendeleza mradi huo,maandalizi ya ujenzi wa mradi Samia Scheme wenye nyumba 100 jijini Dar es Salaam na nyumba 560 eneo la Kawe awamu ya pili yanaendelea kukamilishwa,” amesema
“Nyumba 560 zinaendelea kujengwa katika eneo hilo ambapo hadi kufikia Juni 30,2024 ujenzi wa nyumba hizo umefikia asilimia 65.
Mradi huu wa Kawe utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 48.27 na hadi sasa takribani kiasi cha shilingi biliioni 21.88 zimeshatumika,” amesema
Amesisitiza mauzo ya mradi huo yamefikia asilimia 100 na tayari Shirika limepokea malipo ya awali ya kiasi cha shilingi bilioni 31.2 na kiasi kilichobaki ni shilingi Bilioni 45.5 zinaendelea kukusanywa.
Akizungumzia mradi wa Morocco Square alisema umekamilika kwa asilimia 99 na shughuli za upangishaji tayari umeanza kwa baadhi ya maeneo ikiwemo hoteli yenye vyumba 81 umekamilika na eneo la ofisi za biashara upangishaji unaendelea kukamilika.
Aidha amesema jengo lenye nyumba za makazi 100,tayari nyumba 71 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobaki yanaendelea.
Ameongeza kuwa hadi sasa katika nyumba za makazi na biashara zilizouzwa shirika limekusanya kiasi cha shilingi Bilioni 30 na kiasi cha shilingi Bilioni 35.9 kinaendelea kukusanywa huku eneo la maduka limeshapangishwa kwa asilimia 98 na kwasasa upangaji wa bidhaa unaendelea ili kufungua maduka hayo mwezi julai mwaka huu.
Akizungumza mradi wa Kawe 711,amesema mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 40 ambapo unanyumba 422, pamoja na sehemu za biashara ambao ulianza Novemba 2014 na ulisimama 2018.
Amesema mradi unatekelezwa na mkandarasi Estim Construction Company Limited kwa gharama ya shilingi Bilioni 169.9 na kwa sasa mradi unatarajia kukamilika Aprili 2026.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utali Timotheo Mzava
amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuridhishwa na hatua waliofikia katika utekelezaji wa miradi yake mitatu ikiwemo mradi waSamia Housing Scheme (SHS) uliyopo Kawe jijini Dar es Salaam ambayo inaenda kuacha alama kubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua miradi hiyo, Mzava amesema wanampongeza Rais Samia kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuruhusu NHC kupata fedha ili kuendelea na miradi hiyo.
“Tunalipongeza Shirika letu ya nyumba kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii,” alisema.
Alisema kupitia ziara hiyo kamati imebaini kuwa kazi hiyo isingefanyika vizuri kama siyo nia, moyo, mtazamo na maono ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hasa kutoa kibali kwa NHC kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.” NHC kwa sasa hawana kisingizo tena cha kutokamilisha miradi hiyo kwani tayari fedha zimeshatolewa,”amesema
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuridhia miradi hiyo kuendelea.
Amesema awali miradi hiyo ilisimama kwa muda kupisha mambo ya kiserikali.”mradi wa Morocco Square umeshakamilika kwa asilimia 99 na tayari majengo yaliyopo hapo yameshachukuliwa na wapangaji na wanunuzi kwa asilimia 90 na hiyo ni ishara kwamba miradi sasa inafanyavizuri,”amesema.