Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatoa pongezi za dhati kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa kupata safu mpya ya uongozi wa Rais, Makamu wa Rais na Katibu kwenye uchaguzi uliofanyika tarehe Juni 21, mwaka huu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inawaahidi viongozi hao kuwa itaendelea kutoa ushirikiano kwa Baraza hilo ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kiroho na kijamii kikamilifu kwa ustawi wa Kanisa Katoliki na Taifa letu kwa ujumla.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Mhashamu Wolfgang Pisa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi (Rais), Mhashamu Eusebius Nzigilwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda (Makamu wa Rais) na Padre Charles Kitima Padre wa Jimbo Katoliki la Singida (Katibu Mkuu).
Amesema kuwa kukamilika kwa safu hiyo ya uongozi ndani ya Kanisa Katoliki ni ishara kwamba Kanisa linaendelea kujipambanua juu ya umuhimu wa ngazi za maamuzi zinazosaidia uratibu na usimamizi wa Kanisa.
“Mungu awabariki viongozi wote na kuwasimamia katika majukumu yenu” Amesema Waziri Mkuu.