Watanzania wametakiwa kuendelea kuzingatia ulaji wenye kufuata utaratibu mzuri wa lishe pamoja na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Wito huo umetolewa siku ya Jumamosi Juni 29, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe wakati timu ya wizara hiyo ilipofika katika soko la Bwilingu, lililopo Kata ya Bwilingu, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani kwa lengo la kueneza kampeni ya Mtu ni Afya ambayo amesema kampeni hiyo imejikita katika kubadili tabia za mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla katika kujali afya zao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Ramadhani Possi amesema kuwa kampeni ya Mtu ni Afya imeongeza nguvu katika halmashauri hiyo ambayo tayari ilikuwa na kampeni ya Maji Tiririka huku akiwataka wananchi kuzingatia mambo yaliyo ndani ya kampeni ya Mtu ni Afya ikiwamo kujenga vyoo bora, kuwezesha wasichana na wanawake kumudu hedhi salama bila unyanyapaa, na kutotupa taka hovyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassan Rajabu amesema kuwa wao kama Halmashauri wataibeba ajenda ya Mtu ni Afya kwa nguvu zote ili kuhakikisha usafi unadumu katika Halmashauri hiyo kwani wamehamasika kununua gari na trekta ili kuimarisha afya za wananchi wa Chalinze kwa kuwezesha ukusanyaji, uzoaji na uhifadhi mzuri wa takataka.
Naye Shaban Said Mazengo, Mwenyekiti wa soko la Bwilingu ameonesha kuridhishwa na ugeni kutoka Wizara ya Afya katika kuhimiza masuala mtambuka ya kiafya akieleza kuwa soko hilo lina utaratibu maalumu wa kuzingatia afya hasa uzoaji wa takataka huku akiishukuru serikali kwa kujenga vyoo vya kisasa katika halmashauri hiyo na kuwataka wafanyabiashara, wateja na wananchi wanaofika katika soko hilo kuvitunza vyoo hivyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wanaotumia soko la Bwilingu wameahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usafi unazingatiwa sokoni na hata katika nyumba wanazoishi wakitanabaisha kwamba mtu aliyeshindwa kuzingatia usafi ni sawa na mfanyabiashara aliyeshindwa kulinda mtaji wake.
@wakalawanishativijijini_rea @eucouncil