Wadau wa afya katika Mikoa ya Kagera na Geita Waaswa kulipa madeni wanayodaiwa na MSD, yanayokadiriwa kufikia shilingi bilioni 6.5, ili kuiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake kwa weledi, katika kununua, kutunza, na kusambaza bidhaa za afya, sambamba na kulipa washitiri wanaofanya nao biashara, ili kuufanya mnyororo wa upatikanaji wa bidhaa za afya nchini usikatike, bali uwe endelevu.
Rai hiyo imetolewa hapo jana na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa MSD na Wateja wake, kutoka Mikoa ya Kagera na Geita, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, uliofanyika katika Ukumbi wa ELCT ulioko Manispaa ya Bukoba Mkoani humo.
Mhe. Erasto amesema uwepo wa limbikizo kubwa la madeni linalodaiwa na MSD kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, unaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa taasisi hiyo, hivyo kukwamisha uwezo wake kutoa huduma, kutokana na kuzidiwa na mahitaji kunako sababishwa na uhaba wa fedha.
Katika hatua nyingine Mhe. Erasto amewataka wadau hao kuendelea kushirikiana kwa kuboresha mahusiano na mawasiliano baina yao, ili kwa pamoja waweze kujadiliana na kutatua changamoto mbalimbali zinazo wakabili na kuathiri mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya kwenye maeneno yao.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD Victor Sungusia, amesema MSD imefanya maboresho huduma zake kwa kiasi kikubwa, ikiwemo upatikanaji wa bidhaa za afya ambapo hivi sasa uwezo MSD kukidhi mahitaji ya wateja wake upanda kutoka 40% kwa mwaka 2021/2022, hadi kufikia asilimia 80% kwa mwaka 2023/2024, jambo ambalo limepunguza uhaba wa bidhaa na malalamiko ya wateja.
Bw. Sungusia ameeleza pia jinsi MSD ilivyoboresha jukumu lake la uhifadhi kwa ujenzi wa maghala mapya kwenye kanda zake nchini, ambapo hivi sasa ujenzi wa maghala kwenye kwenye kanda za Dodoma, Mtwara unaendelea kwa bajeti ya fedha ya m waka 2023/2024 na kuanzia mwaka ujao
wa fedha maghala kwenye kanda za Kagera na Mwanza unatazamiwa kuanza.
Katika hatua nyingine Bw. Sungusia amebainisha jinsi MSD ilivyoboresha usambazaji wa bidhaa za afya nchini, kutoka mara 4 hadi kufikia mara 6 kwa mwaka, ambapo zoezi hilo hufanyika kila baada ya miezi miwili, huku maboresho hayo yakielezwa kuimarisha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Kagera Masatu Kalendero amewashukuru wadau hao kwa ushirikiano wao, huku akiahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizoibuliwa huku akiwashi wadau hao kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano, ili kwa Pamoja waweze kuboresha afya kwa wananchi.